Habari za Kitaifa

Matrela sasa yatumika kulangua bangi

June 9th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

MAKACHERO kutoka kitengo cha kupambana na mihadarati kanda ya Pwani wamemkamata mwanamume wa umri wa miaka 27 akilangua bangi kwa kutumia lori la trela lililokuwa likitoka Busia kuelekea jijini Mombasa.

Maafisa hao walizuia lori hilo lililokuwa na magunia ya bangi katika eneo la Kibaokiche kando ya barabara ya Mariakani–Mavueni mnamo Jumamosi saa tisa alfajiri.

Bw Auress Godfrey Otieno, anayedaiwa kuwa ni mwanafunzi wa chuo kikuu, alikuwa na magunia saba ya bangi yenye uzito wa kilo 429.3 na ambayo inakisiwa ni ya thamani ya Sh12.8 milioni.

Dereva wa lori lililokuwa limeibeba, Bw Joseph Nzomo, pia alikamatwa.

Akihutubia wanahabari afisini mwake, Afisa wa Uchunguzi wa Jinai (DCIO) katika Kaunti ya Kilifi Bw David Siele alisema mshukiwa, Bw Otieno, alikuwa muuzaji wa bangi aliyekuwa kwa rada ya makachero wakimsaka.

“Tumekuwa tukifuatilia mienendo ya mtuhumiwa kwa sababu tulikuwa tunafahamu aina ya biashara ambayo anafanya na tulikuwa tukimfuatilia. Lori hilo lilikuwa likiendeshwa kutoka Busia hadi Mombasa lakini likaingia Mariakani kushukisha bangi,” alisema Bw Siele.

Afisa huyo alisema maafisa wa upelelezi walikuwa na habari kuhusu mpango wa Bw Otieno kupokea shehena yake na wakavizia kumnyaka.

“Wapelelezi walifanikiwa kulinasa lori hilo la trela la Mercedes Benz lenye nambari za usajili KAY 269J ambalo lilinakiliwa katika Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai Kilifi kwa uchunguzi na pia wakaanza matayarisho ya kujenga kesi ambapo washukiwa hao watafikishwa mahakamani Jumatatu,” alisema.

Bw David Siele akihutubia wanahabari. PICHA | MAUREEN ONGALA

Bw Siele alisema mshukiwa mkuu, Bw Otieno, aliagiza bangi na alifuata lori hilo kuchukua kifurushi chake.

“Bw Otieno anatoka Mombasa na alikuwa ameagiza mizigo yake na alikuwa amelifuata lori ili kulielekeza hadi pahali pa biashara haramu,” akasema.

Afisa huyo wa Upelelezi wa Jinai katika Kaunti ya Kilifi alibaini kuwa wafanyabiashara hiyo sasa wana mtindo kutumia malori ya matrela kusafirisha bangi yakirudi katika bandari ya Mombasa.

“Ni mtindo mpya ambao wafanyabiashara wa dawa za kulevya wameukumbatia, kulingana na wamiliki wa matrela wanaosema madereva hao wanatumiwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hiyo hadi Mombasa,” aliongeza.

Malori hayo kila mara hupakua magunia ya bangi kwenye yadi maarufu ya Kibaokiche na kisha inachukuliwa na magari madogo ya kibinafsi kupelekwa maeneo mbalimbali.

Bw Auress Otieno,27, (kati kushoto) ambaye inadaiwa ndiye mmiliki wa magunia saba ya bangi na dereva wa lori la trela Bw Joseph Nzomo walipokamatwa katika eneo la Kibaokiche katika barabara ya Mariakani-Mavueni mnamo Juni 8, 2024. PICHA | MAUREEN ONGALA

Magari hayo ya kibinafsi huwa yanangoja lori kufika kwa yadi.

Baadhi ya magunia ya bangi huachwa kando ya barabara kuu wakati malori hayo yakielekea Mombasa.

Bw Siele alisema mnamo Machi 5, 2024, maafisa wa upelelezi walinasa lori lililokuwa na magunia saba ya bangi huko Mariakani.

“Maafisa wetu wako macho, tunafuatilia na tunaimarisha vita vyetu ili bangi hii isifike mitaani na kuwaharibu vijana wetu,” alisema.

Mnamo 2022, polisi kutoka Kaunti Ndogo ya Rabai walinasa lori katika eneo la Kokotoni kando ya barabara kuu ya Nairobi-Mombasa likiwa na magunia 16 ya bangi ya uzito wa kilo 825 na ambayo thamani yake ilikuwa ni Sh25.5 milioni.

Lori hilo lilikuwa linatoka Uganda kuelekea jijini Mombasa.