Afya na Jamii

Mbinu ya kukabili uvimbe wa ‘fibroid’ unaoathiri wanawake wengi


WANAWAKE wengi watakiri kuwahi kukumbwa na tatizo la uvimbe wa ‘fibroid’.

Fibroid ni uvimbe ambao japo hausababishi kansa, sio wa kawaida.

Uvimbe huu huota kwenye uterasi ya mwanamke katika miaka yake ya uzazi. Kulingana na utafiti, asilimia 80 ya wanawake hukumbwa na uvimbe wa fibroid wanapotimu miaka 50.

Mojawapo ya mbinu za kimatibabu ambazo hutumika kukabiliana na hali hii ni uterine fibroid embolization (UFE).

Utaratibu huu hausababishi maumivu na unahusisha mwongozo wa picha ambapo tayari umefanyiwa wagonjwa wengi humu nchini.

Manufaa makuu ya utaratibu huu kwa wanawake ni kwamba mkato ni wa ukubwa wa milimita 2 na kwamba wanaweza kurejea kazini katika kipindi cha wiki moja baada ya kufanyiwa utaratibu huu.

Utaratibu wa UFE hutekelezwa na mwana rediolojia ambaye huingiza mrija mdogo kwenye mkato mdogo wa ukubwa wa milimita 2 juu ya mguu, au kwenye kifundo cha mkono, na kuusukuma kwa utaratibu kupitia ateri ya uterasi, kisha kuingiza chembe chembe ndogo kwenye ateri zinazosambaza damu kwa uterasi na uvimbe wa fibroid.

Chembechembe hizi huzuia usambazaji wa damu kwenye fibroid, na hivyo kusababisha uvimbe huu kunywea na kufa.

Utaratibu huu ni salama kwa wanawake wanaotaka kushika mimba baada ya kufanyiwa UFE, japo huwa inashauriwa kuwa mtu asubiri kwa kati ya miezi sita na mwaka mmoja, kabla ya kujaribu kushika mimba.