• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 6:50 PM
JIJUE DADA: Chanzo cha vidutu kwenye tupu ya nyuma

JIJUE DADA: Chanzo cha vidutu kwenye tupu ya nyuma

NA PAULINE ONGAJI

VIDUTU (warts) vyaweza tokea katika sehemu yoyote mwilini.

Kuna vidutu vinavyofahamika kwa jina anogenital warts, ambavyo husababishwa na virusi vya Human Papilloma Virus (HPV).

Mara nyingi vidutu hivi husambazwa kwa njia ya kujamiiana. Hata hivyo, kuna baadhi ya watu wanaokumbwa na vidutu hivi pasipo kushiriki ngono.

Hii hutokea ikiwa utakuwa na mgusano wa moja kwa moja na mtu aliye na vidutu hivi kisha ujiguse katika sehemu hizi.

Pia, virusi vya HPV vyaweza sambaa hata ikiwa hakuna vidutu vinavyoonekana kwenye ngozi ya mtu aliye navyo.

Vidutu vingi vya aina hii havina uchungu. Hata hivyo, vidutu vikubwa kwenye tupu ya nyuma vyaweza kumkosesha mwathiriwa starehe.

Mara nyingi husababisha kutokwa na majimaji mfano wa ute sehemu hii, na mwasho. Mwasho waweza sababisha nyufa katika ngozi na hata damu kuvuja, na wakati mwingine maambukizi katika sehemu husika.

Utambuzi huhitaji uchunguzi wa kimatibabu. Mara nyingi daktari wako atavitambua kwa kuviangalia. Ikiwa kuna wasiwasi kwamba uvimbe huu waweza sababisha kansa, basi huenda daktari akafanya uchunguzi wa seli na tishu (biopsy). Aidha, daktari ataangalia ndani ya tupu yako ya nyuma kubaini iwapo pia vimeota mle ndani.

Uko katika hatari kubwa ya kuambukizwa na kusambaza vidutu hivi ukishiriki ngono bila kinga, kushiriki ngono na watu tofauti, ukianza kushiriki tendo la ndoa katika umri mdogo, kushiriki ngono na mtu aliye na virusi vya HPV (hata ikiwa hawana vidutu vinavyoonekana), ukijamiiana kupitia tupu ya nyuma au ikiwa kingamwili yako ni dhaifu.

Kuna chanjo dhidi ya HPV. Chanjo hii hutolewa kwa wanawake hadi umri wa miaka 45 ambapo imetambulika kupunguza matatizo yanayotokana na HPV kama vile kansa ya lango la uzazi/tupu ya nyuma na hata vidutu.

You can share this post!

MUME KIGONGO: Mazoezi magumu kupindukia hupunguza hamu ya...

Kocha wa Harambee Starlets ana kibarua kuteua timu ya mwisho

T L