Habari za Kitaifa

Mbunge John Kiarie aomba Gen Z msamaha kwa matamshi yake telezi

Na LABAAN SHABAAN June 24th, 2024 1 min read

IMEBIDI Mbunge wa Dagoretti Kusini, John Kiarie maarufu kama KJ aliyekejeli maandamano yanayoendeshwa na vijana wa kizazi cha kisasa (Gen Z) atafune maneno yake.

Juma lililopita, Bw Kiarie aliropoka bungeni akisema picha za matukio ya maandamano zilizosambazwa, wakati Gen Z walijaa mitaani kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, zilikuwa ghushi.

“Kwa moyo mkunjufu, ninaomba msamaha kwa kauli niliyotoa kuhusu uhalali wa picha za maandamano. Wakati wa mjadala wa Mswada wa Fedha, maneno yangu hayakuwa na maana, yalikosa msingi na hayakuwa yenye kujali hisia za wengine,” alisema Bw Kiarie kupitia barua aliyoandika kwa mkono na kupachika kwenye akaunti zake za mitandao wa kijamii.

“Ninajutia sana niliyoyasema baada ya kutafakari na pia kuelewa hasira na matukio ya kukata tamaa yanayoshuhudiwa nchini. Ni ghadhabu za matatizo ya miaka mingi bila suluhu kuhusiana na masuala muhimu ya taifa,” aliongeza.

Kitumbua cha mbunge huyu kiliingia mchanga baada ya kusema picha zilihaririwa na kurushwa mitandaoni kuonyesha maandamano yamechacha nchini.

KJ pia alidokeza kuwa watumiaji mitandao walikusanya picha za maandamano ya sehemu tofauti duniani na kuzipachika kwenye majukwaa ya kijamii.

“Baadhi ya picha mnazoona, nitawaambia kwa sababu mimi ni msanifu wa grafiki, kuwa si za Kenya,” aliwaka.

“Mimi ni mhariri wa picha na ninaweza kutambua zile zilizohaririwa kuonekana kama ni za maandamano ya Gen Z.”

Kauli hii iliwapandisha mori wananchi ambao waliona kuwa KJ hajali hisia zao.

Hapo ndipo wakaanza kumshambulia kwenye mitandao ya kijamii hadi akaamua kuomba msamaha.

Mbunge huyu aliyechaguliwa kupitia tikiti ya chama cha UDA, ameonekana kubadili kauli hasa baada ya Rais William Ruto Jumapili, Juni 23, 2024 kuashiria kusalimu presha ya vijana wanaoandamana.

Rais Ruto, ambaye pia ndiye kinarwa wa UDA na muungano tanzu wa Kenya Kwanza, alisema kwamba yuko tayari kuzungumza na vijana ili kuangazia masaibu yao.