Habari za Kitaifa

Mvua kubwa kurejea tena nchini kuanzia Jumanne, Idara yatangaza

May 20th, 2024 1 min read

Na HILLARY KIMUYU

IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa imetoa tahadhari kuwa mvua kubwa itanyesha nchini kuanzia Jumanne, Mei 21, 2024.

Kwenye utabiri huo, idara hiyo imeonya kuwa mvua kubwa yenye upepo mkali itashuhudiwa maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hilo, wananchi wametakiwa wakae ange na kutahadhari sana kwa sababu mafuriko yanatarajiwa kutokea.

Kwa mujibu wa idara hiyo, mvua zaidi ya milimita 30 inatarajiwa ndani ya saa 24 zinazokuja katika maeneo mbalimbali nchini.

Kati ya maeneo hayo ni Ukanda wa Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Milima ya Mashariki na Magharibi ya Bonde la Ufa na Nairobi.

“Mvua hiyo kubwa itakuwa zaidi ya milimita 40 katika maeneo hayo kuanzia Mei 20-21, 2024. Inaweza kupungua baada ya Jumatano ila itaendelea Pwani hadi Ijumaa,” ikasema taarifa ya Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo, Dkt David Gikungu.

Kaunti ambazo zitaathirika na mvua hiyo ni Kisumu, Homabay, Siaya, Migori, Busia, Kisii, Nyamira na Nandi.

Nyingine ni Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Narok, Baringo, Nakuru, Trans-Nzoia na Uasin-Gishu.

Magatuzi mengine ni Elgeyo-Marakwet, West-Pokot, Turkana, Samburu, Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Nairobi, Machakos, Kajiado, Mombasa, Tana-River, Kilifi, Lamu na Kwale.

“Wakenya wanashauriwa wajizuie kuyaendesha magari au kutembea majini na pia wajizuie kujikinga chini ya miti au vifaa vya chuma. Hii itazuia tukio ambalo watapigwa na radi,” akaongeza Dkt Gikungu.