Habari Mseto

Mvutano wachacha MCAs wakimtimua kiongozi wa wengi

June 12th, 2024 2 min read

NA PIUS MAUNDU

TAHARUKI ilitanda katika Bunge la Kaunti ya Makueni kwa siku ya pili Jumanne baada ya kundi la madiwani wa chama cha Wiper, kumtimua Kiongozi wa Wengi katika bunge hilo.

Walinzi katika bunge hilo walitazama huku baadhi ya madiwani wakizomea na kujaribu kumtimua kiongozi huyo katika bunge hilo.

“Wewe si kiongozi wetu wa walio wengi,” mmoja wa madiwani alipaza sauti akiungana na wenzake kujaribu kumtimua diwani wa Wadi ya Tulimani, Bw Kyalo Mumo ambaye amekuwa Kiongozi wa Walio Wengi katika bunge tangu 2017.

Nje ya majengo ya bunge hilo, wahudumu wa boda boda waliokuwa wamebeba mabango ya kukashifu uongozi wa Bw Mumo walizua taharuki.

Matatizo yalianza Jumatatu baada ya kundi la madiwani 13 wa Wiper kutoka katika mkutano waliofanya katika hoteli ya Makueni na kutangaza kuwa wamemtimua Bw Mumo kama kiongozi wa wengi.

Katika mabadiliko hayo, ambayo Spika wa Bunge la Makueni, Bw Douglas Mbilu hakuwa ameidhinisha kufikia Jumanne, diwani wa wadi ya Kithungo/Kitundu, Bw Kisungi Katete, alichukua nafasi ya Bw Mumo kama Kiongozi wa Wengi huku diwani wa Nzaui/Kilili/Kalamba, Bw Francis Mutuku, akipoteza nafasi ya naibu Kiongozi wa Wengi kwa mwenzake wa Ilima, Bw Jonathan Muthoka.

Wengine walioathirika katika mabadiliko hayo ni Bi Magdalene Mulwa ambaye alikuwa kiranja wa wengi. Nafasi yake ilichukuliwa na Bi Joyce Mwende.

Mrengo wa madiwani wa Wiper unaoongozwa na Bw Katete, unajumuisha hasa walioteuliwa ambao wanashutumu uongozi wa bunge kwa ubaguzi katika kutoa marupurupu.

Pia wanashutumu uongozi wa wengi kwa kutokuwa na nia ya kumpigia debe kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka kama mgombeaji wa urais katika kaunti hiyo.

“Mrengo unaoongozwa na Bw Mumo haujawa na nia ya kuendeleza ajenda ya Wiper. Wanachama wa Wiper wamekutana mara tatu pekee tangu Agosti 2022. Wamekuwa wakifanya mikutano na maajenti wa United Democratic Alliance (UDA),” diwani wa Wiper, Bw Urbanus Wambua alisema.

Mrengo wa Bw Mumo ulipuuzilia mbali shtuma hizo huku ukiwashutumu viongozi hao wapya.

“Mabadiliko yanayodaiwa katika uongozi wa wengi katika bunge la kaunti ni batili. Kundi hilo halikufuata kanuni za bunge wakati wa kujichagua wenyewe. Sheria inawataka wanachama wanaolalamika kuandika barua kwa uongozi wa bunge kabla ya kufanya uchaguzi,” aliwaambia waandishi wa habari katika majengo ya bunge la kaunti kabla ya mabishano na kurushiana makonde na mrengo wa pili kuvuruga mkutano huo.