Habari za Kitaifa

Orengo ajitetea vikali dhidi ya madai ya kumdhalilisha Oduol

May 24th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

GAVANA wa Siaya James Orengo amekana madai ya kumdhalilisha Naibu wake William Oduol kwa kuhujumu ofisi yake na kumteua diwani wa wadi ya Siaya Mjini Obiero Atare kuwa ‘kaimu naibu gavana’.

Akijitetea Alhamisi mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi baada ya Dkt Oduol kuwasilisha malalamishi yake, Bw Orengo alisema hana mamlaka ya kumdhulumu naibu wake kwani mamlaka ya ofisi hiyo yanalindwa na Katiba.

“Ukweli ni kwamba chimbuko la masaibu ya naibu wangu ni siasa. Aliamua kinyume na matakwa ya wakazi wa Siaya kubadili msimamo wake kisiasa na hivyo kupoteza imani ya wananchi,” akasema Bw Orengo.

“Ningependa kuiambia kamati hii kwamba hata mimi nikiamua kubadili msimamo na kukumbatia na kuuza sera za chama kingine cha kisiasa katika Kaunti ya Siaya mbali na Orange Democratic Movement, wakazi na viongozi wote watanikataa,” Bw Orengo akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Wajir Abbas Mohamed.

Gavana wa Siaya James Orengo. PICHA | CHARLES WASONGA

Baada ya kuponyoka kutimuliwa Juni 2023, Dkt Oduol amekuwa akiupigia debe mrengo tawala wa Kenya Kwanza.

Awali, Dkt Oduol aliwaambia wanachama wa kamati hiyo kwamba Bw Orengo amekuwa akimdhalilisha na kumzuia kutekeleza majukumu yake tangu Juni 27, 2023, hoja ya kumtimua ofisini ilipotupiliwa mbali na Seneti.

“Gavana Orengo alikiuka agizo la Bunge hili la Seneti kwamba aniruhusu nitekeleze majukumu ya ofisi yangu bila vikwazo vyovyote baada ya hoja ya kunitimua kuangushwa. Badala yake, alinikoponya gari la kazi, amezuia gari langu rasmi kuwekewa mafuta na amenizima kuhudhuria vikao vya Baraza la Mawaziri wa Kaunti,” akasema.

“Isitoshe, ameteua Diwani wa wadi ya Siaya Mjini Obiero Otare kuwa kaimu Naibu Gavana wa Siaya kinyume na Katiba,” Dkt Oduol akadai.

Naibu huyo wa Gavana aliwaambia maseneta kwamba anapojaribu kuhudhuria mikutano ya baraza la mawaziri wa kaunti, Bw Orengo hutuma walinzi wake na ‘genge la wahuni’ kumfurusha.

“Isitoshe, nimekuwa nikitumia pesa zangu binafsi kununua mafuta ya gari langu rasmi ninapotekeleza wajibu wangu wa kukagua miradi ya maendeleo katika Kaunti ya Siaya,” Dkt Oduol akawaambia maseneta.

Naibu Gavana wa Siaya Dkt William Oduol. PICHA | CHARLES WASONGA

Lakini Bw Orengo alipinga madai hayo akieleza kuwa mafuta ambayo gari rasmi la Dkt Oduol hutumia hununuliwa na serikali ya Kaunti ya Siaya.

“Katika stakabadhi ambazo nimewasilisha mbele yenu, nimeambatanisha risiti zilizotiwa saini na dereva wa Dkt Oduol kuthibitisha kwamba gharama ya mafuta yanayotumika na gari lake hulipiwa na serikali ya kaunti,” akasema.

Aidha, Bw Orengo alipuuzilia mbali madai ya Dkt Oduol kwamba amedinda kumpa majukumu akisema baada ya wao kuingia ofisini, alimpa Naibu wake wajibu wa kusimamia utendakazi wa Wizara ya Fedha.

“Kupitia taarifa, niliamuru kuwa Waziri wa Fedha katika Kaunti ya Siaya awe akiripoti kwa ofisi ya naibu wangu. Vilevile, nilimteua kuwa mwenyekiti wa Kamati ya kukagua zabuni zote zinazotolewa na serikali ya kaunti,” Bw Orengo akaeleza.

Tofauti kati ya Gavana Orengo na Naibu wake zilianza tangu mapema 2023, pale Dkt Oduol alipoibua madai ya ufisadi na ubadhirifu wa pesa za umma katika Kaunti ya Siaya.

Mvutano huo, ulisababisha madiwani wa kaunti hiyo, wengi wao wakiunga mkono Gavana Orengo, kupitisha hoja ya kumtimua ofisini mnamo Mei 2, 2023.

Hata hivyo, hatua hiyo ilibatilishwa na Seneti mnamo Juni 27, 2023, baada ya maseneta 27 (wengi wao kutoka mrengo wa Kenya Kwanza) kupiga kura ya kutupilia mbali hoja hiyo. Ni maseneta 16 pekee, wengi wao wakiwa wa mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya, waliounga mkono hoja hiyo.