Michezo

Oslo Diamond League: Cheruiyot kufufua uhasama na Ingebrigtsen

May 30th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia mbio za mita 1,500 mwaka 2019, Timothy Cheruiyot, atafufua uhasama na mwenyeji Jakob Ingebrigtsen kwenye duru ya Diamond League jijini Oslo, Norway, Alhamisi usiku.

Wakenya Caroline Nyaga, Edinah Jebitok (3,000m), Stanley Waithaka (5,000m) na Boaz Kiprugut (1,500m) pia wanashiriki duru hiyo inayokuja baada ya Xiamen, Shanghai/Suzhou, Doha, Marrakech na Eugene.

Cheruiyot anajivunia ushindi mara 11 dhidi ya saba ya Ingebrigtsen, ingawa afisa huyo kutoka Idara ya Magereza hajaonja ushindi dhidi ya Ingebrigtsen mara nne mfululizo.

Mkenya Timothy Cheruiyot akiingia uwanjani kushiriki mbio za mita 1500 katika siku ya 15 ya Michezo ya Olimpiki ya Tokyo 2020 katika Olympic Stadium mnamo Agosti 7, 2021. PICHA | MAKTABA

Wawili hao walikutana mara ya mwisho wakati wa Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary wakati Ingebrigtsen alitwaa medali ya dhahabu kwa kukamilisha mizunguko hiyo mitatu kwa dakika 3:34.98 naye Cheruiyot akakamata nafasi ya tisa kwa 3:37.40.

Wote wanafukuzia ushindi wa kwanza msimu huu baada ya Cheruiyot kuwa nambari mbili katika 1,500m kwenye duru ya Doha nchini Qatar naye Ingebrigtsen akawa pia wa pili nyuma ya Josh Kerr mjini Eugene, Amerika.