Habari za Kitaifa

Polisi walivyowaua watu kikatili Githurai

Na NDUBI MUTURI June 30th, 2024 2 min read

SOKOMOKO zilishuhudiwa eneo la Githurai 45, kaunti ya Kiambu Jumanne jioni wiki hii polisi walipowashambulia wakazi kwa risasi kiholela baada ya maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Watu ambao idadi yao haijulikani walikufa katika patashika hilo akiwemo makanga wa matatu aliyetambuliwa kama, Mcoast.

Wakati wa fujo hizo, wakazi wa eneo hilo, lenye shughuli nyingi, walikwepa risasi ambazo polisi walikuwa wakifyatua kutoka kwa daraja la juu.

Walioshuhudia kisa hicho walisema hakijawahi kuonekana katika miaka ya nyuma.

“Kulikuwa na fujo kila mahali. Baadhi ya watu walijificha ndani ya soko kukwepa risasi za polisi. Barabara haikuweza kupitika,” Martin Njeri, ambaye ni mhudumu wa bodaboda akaambia Taifa Leo.

Video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii iliwaonyesha watu wakikimbia kujisalimisha milio ya risasi ikisikika hewani.

Polisi walisema walifyatua risasi 740 za mipira, risasi 18 halisi na mikebe 958 ya vitoa machozi kuwatawanya zaidi ya waandamanaji 6,000 ambao walianza kuzua fujo baada ya kudumisha amani majira ya asubuhi.

“Vitoa machozi vililipuliwa kuwatawanya lakini maafisa hao waliwalemea hadi wakaamua kuondoka ha hapo ndipo waandamanaji waliziba barabara kwa nguzo za stima na kisha wakateketeza gari la polisi lenye nambari ya usajili; GKA 601L,” ikasema taarifa kutoka kwa polisi.

Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Faith Odhiambo amependekeza kuwa uchunguzi huria uendeshwe kuhusu tukio la Jumanne, Juni 25 katika mtaa wa Githurai.

“Tunatoa wito wa jamii ya kimataifa kuendesha uchunguzi kuhusu mauaji ya raia yaliyotekelezwa na polisi katika mtaa wa Githurai Jumanne usiku. Mbona mauaji yalitekelezwa mahala ambapo watu huishi kwa amani? Tunahitaji majibu kwa maswali haya,” akasema Jumatano kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi.

Akaongeza: “Katika mitandao ya kijamii, watu wanasema kuwa zaidi ya watu 100 waliuawa. Kwa hivyo, watu waliosababisha vifo hivyo sharti waadhibiwe,” akaongeza.

Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu (KNHCR) Ijumaa ilisema kuwa ilithibitisha vifo vya watu 23, wakiwemo 19 kutoka katikati mwa jiji la Nairobi, wakati wa fujo hizo za Jumanne.

Baadhi ya wakazi wa Githuria 45 walisema watu wengi waliuawa lakini walihofia kutoa idadi kamili wasije wakaandamwa na polisi.