Habari Mseto

Presha Ukambani nao wapige marufuku muguka

June 10th, 2024 2 min read

Na PIUS MAUNDU

MAGAVANA wa Kaunti za Kitui, Machakos na Makueni sasa wameelekezewa shinikizo za kupiga marufuku muguka huku viongozi wa kidini na wa kijamii wakisema mmea huo una athari za kiafya na kiuchumi.

Aliyekuwa Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana amewataka wanasiasa wote washirikiane kupiga marufuku kilimo, biashara na matumizi ya muguka.

Shinikizo za kuharamisha matumizi ya muguka Ukambani zinakuja wakati ambapo wito umetolewa kwa serikali kuwatumia machifu na polisi kuwalinda wanaoshiriki kilimo cha miraa na muguka.

“Viongozi wa Ukambani wanastahili kupaaza sauti yao kuhusu muguka. Muguka ni hatari sana kwa watoto wetu,” akasema Profesa Kibwana wakati wa hafla ya mazishi katika Shule ya Msingi ya Nduundune.

Kauli yake ilikuja baada ya Gavana Wavinya Ndeti kukiri kuwa anakabiliwa na shinikizo za kupiga marufuku muguka katika kaunti za Pwani ambazo zimepiga marufuku biashara ya muguka.

Bi Ndeti hata hivyo, alisema kuwa serikali yake haitachukua hatua na kupiga marufuku muguka kwa kuwa bado mashauriano yanaendelea kuhusu suala hilo.

“Napanga kushauriana na watu kuhusu muguka kwa kuwa siwezi kuangusha marufuku hiyo kivyangu. Matokeo ya mashauriano hayo ndiyo yatatoa mwelekeo kuhusu suala hili,” akasema Bi Ndeti.

Kongamano lililoandaliwa na washikadau kuhusu kilimo cha miraa na muguka katika hoteli moja mjini Machakos, kulishuhudia Magavana Cecily Mbarire (Embu) na Kawira Mwangaza (Meru) wakimtaka Rais William Ruto aingilie suala hilo.

“Tunaomba Rais William Ruto aingilie suala hili la muguka kwa sababu marufuku ambayo imewekwa inaathiri moja kwa moja maisha ya wakazi wanaotegemea kilimo hiki,” akasema Bi Mbarire. Mkutano huo ulisusiwa na magavana kutoka Pwani ambao wanasisitiza kuwa muguka haitauzwa maeneo yao.

Bi Mbarire na Mwangaza walitoa wito kwa serikali iwatumie machifu na polisi kuwalinda wanaofanyabiashara ya muguka.

“Wizara ya Usalama wa Ndani inastahili kutekeleza amri ya mahakama ya Mei 28, 2024 kuwa wakulima wa miraa na muguka walindwe na wasihangaishwe kwenye kaunti ambako mmea huo ushapigwa marufuku,” akasema Bi Mbarire.

Kwenye taarifa, magavana wa kaunti za Kwale, Kilifi, Lamu, Mombasa, Taita Taveta na Tana River waliitaka Shirika la Kupambana na Dawa za Kulevya (NACADA) na Wizara ya Afya, zijumuishe muguka na miraa kama dawa za kulevya.

Katibu katika wizara ya Kilimo Kiprotich Rono naye alitoa wito kwa suluhu ya haraka ipatikane kuhusiana na mzozo unaoendelea wa mauzo ya muguka.