Afya na Jamii

Sababu za korongo kuondoka Ziwa Nakuru

February 13th, 2024 4 min read

NA PAULINE ONGAJI

KWENYE ufuo wa Ziwa Nakuru, Bw Nicholas Rioba, mkazi wa eneo la Lunga Lunga, Kaunti ya Nakuru, anafurahia mandhari murwa ya maji kabla ya kusimama ghafla na kuokota ubawa wa korongo uliochakaa.

Hali ya ubawa huu inaashiria taswira kamili ya jinsi ndege hawa wamekuwa wakitoweka katika ziwa hilo kwa miaka kadhaa sasa, sawa na baadhi ya maziwa mengine ya Bonde la Ufa, hapa nchini.

“Nakumbuka katika miaka ya themanini ziwa hili lilikuwa kivutio kikuu hasa kwa watalii waliokuwa wakimiminika hapa kufurahia ndege hawa waliokuwa wengi,” akumbuka Bw Rioba.

Lakini miaka ilivyozidi kusonga, ndivyo idadi ya ndege hawa ilivyozidi kupungua. Kudorora kwa kwa ndege hawa nako kumepunguza kabisa idadi ya watalii wanaozuru eneo hili, na hivyo kuathiri pakubwa nafasi za ajira.

“Ombi langu ni kwamba hatua ichukuliwe na kurejesha fahari ya ziwa hili kama ilivyokuwa miaka ya awali,” aongeza Bw Rioba.

Idadi ya korongo imepungua

Tangu mwaka wa 2011 idadi ya korongo katika Ziwa Nakuru imepungua kabisa, huku ndege hawa wakiendelea kuhamia maeneo mengine.

Kwa kawaida, Makavazi ya Kitaifa nchini, Huduma ya Kitaifa ya Wanyamapori, Shirika la Nature Kenya na washikadau wengine, hushirikiana kuhesabu idadi ya ndege majini, shughuli ambayo hufanyika mara mbili kila mwaka.

Kati ya mwaka wa 2008 na 2015, takwimu za hesabu hasa katika Maziwa ya Nakuru na Bogoria, zilifichua kwamba idadi ya korongo ilikuwa ikipungua kwa kasi mno.

Kufikia Januari 2021, takwimu kutokana na hesabu hizi zilionyesha kwamba idadi ya korongo ilikuwa inakaribia 6,000 pekee katika Ziwa Nakuru, huu ukiwa upungufu mkubwa ikilinganishwa na mwaka wa 2000 ambapo idadi ya ndege hawa ilikuwa inakaribia milioni moja.

“Mwezi Oktoba mwaka jana, tulihesabu ndege hao na tukapata kwamba idadi yao ilikuwa chini ya 100,” asema Bw Jared Lumbasi, mtafiti mkuu katika Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Wanyamapori (WRTI).

Uhamiaji wa ndege hawa kuelekea katika maziwa mengine ya Bonde la Ufa kama Ziwa Bogoria na Ziwa Natron, ulihusishwa na ongezeko kubwa la usawa wa bahari katika Ziwa Nakuru, ambalo kwa kawaida lilikuwa la maji ya chumvi.

Kulingana na wataalamu wa ndege na wahifadhi wa mazingira, ongezeko la usawa wa maji ziwani umeathiri sana makazi asili ya ndege hawa.

“Ongezeko la viwango vya maji umezimua maji katika ziwa hili, na hivyo kuathiri pakubwa ukuaji wa ukuvu wa kijani kwa jina spirulina.

Ukuvu wa Spirulina

Baadhi ya vidimbwi ambavyo vimejengwa kwa lengo la kukuza spirulina ambacho ndicho chakula cha Korongo. PICHA|
PAULINE ONGAJI

“Ukuvu wa spirulina ndio chakula kikuu cha korongo,” aeleza Bw Timothy Mwinami, mtafiti wa ndege katika Makavazi ya Kitaifa nchini.

Kwa kawaida, ukuvu wa spirulina huota katika mazingira ya maji ya chumvi kwenye maziwa ya Bonde la Ufa, ikiwa ni pamoja na Ziwa Nakuru.

Kwa mujibu wa Bw Mwinami, kuendelea kutoweka kwa chakula hiki cha korongo kumechangia kuendelea kupungua kwa idadi ya ndege hawa.

Wataalamu wamehusisha hali hii na mabadiliko ya tabianchi.

“Katika kipindi cha mwongo mmoja uliopita, mfumo wa ikolojia wa Ziwa Nakuru umepitia mabadiliko makubwa ambayo yamehusishwa na mabadiliko ya tabianchi. Mojawapo ya mabadiliko hayo ni kufurika kwa maji baridi hasa kutoka Mto Njoro,” aeleza Bw Lumbasi.

Lakini hata mambo yanavyoendelea kuonekana mabaya, huenda kukawa na matumaini kwani Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Wanyamapori (WRTI), inapanga kuanzisha mradi wa kipekee ili kujaribu kufufua kiwango cha ukuvu wa spirulina katika ziwa hili.

Shirika la WRTI linapanga kukuza aina fulani ya ukuvu wa spirulina ulio katika familia ya cynobacteria na kuutia ziwani kila mara, huku wakitumai kwamba endapo idadi ya mimea hii itaongezeka, basi korongo watavutiwa na kurejea katika Ziwa Nakuru.

“Tuko katika harakati za kuzalisha ukuvu wa spirulina kwenye vidimbwi, ambapo mpango wetu ni kuwa tutakuwa tukichukua mimea hii na kuiweka ziwani, na hivyo kuunda mazingira yanayofaa kwa korongo,” aeleza Bw Lumbasi.

Bw Lumbasi asema, tayari miundo misingi imewekwa.

“Tuna vidimbwi viwili ambavyo viko tayari kupokea mimea ya spirulina, na pia mbegu zinafanyiwa utafiti katika maabara huku tukijitahidi kutafuta uzao bora zaidi.”

Vidimbwi vipana

Kwa mujibu wa mtaalamu huyu, kwa kawaida wao huunda vidimbwi vipana ambapo mchanganyiko wa chumvi na virutubishi hutiwa mle, kabla ya mchanganyiko huo kukorogwa na hivyo kuwezesha ukuvu huo kuota na kujizidisha kwa idadi.

“Ukuvu wa spirulina huota vyema katika mazingira yaliyo na pH ya kuanzia 9 na zaidi, kumaanisha kwamba katika harakati zetu za kuukuza, tunajaribu kuunda mazingira sawa na yale yanayopatikana katika maskani halisi, ambayo ni maji ya chumvi.”

Kwa kawaida huchukua wiki moja kwa ukuvu wa spirulina kuota, na hivyo wanatumai kwamba pindi watakapoanza kuzalisha mimea hii, itaendelea kuota ambapo wanatarajia kuvuna mara moja kwa wiki na kuiweka kwenye Ziwa Nakuru.

“Kidimbwi kimoja kina uwezo wa kulisha korongo 50, lakini kuna mipango ya kuimarisha kiwango cha ukuzaji kwa kufanya kazi na uzao unaoota kwa wingi,” aongeza Bw Lumbasi.

Kufikia mwisho wa hayo yote, mtaalamu huyu asema kwamba wanatumai kuimarisha kiwango cha ukuvu wa spirulina, na hivyo kuimarisha mfumo wa ikolojia katika Ziwa Nakuru, na hatimaye kuvutia idadi kubwa ya korongo.

Mpango kufanikiwa

Lakini hata wanavyoendelea na mipango hii, kuna baadhi ya wataalamu walio na tashwishi kuhusu iwapo mpango huu utafanikiwa.

Kulingana na Bw Mwinami, kutokana na sababu kwamba viwango vya PH vitasalia sawa ziwani, inamaanisha kwamba huenda halijoto ya mazingira ikawa juu au chini ya kiwango kinachostahili.

“Inachukua saa chache sana kwa ukuvu huu kuangamia katika mazingira yasiyofaa, kumaanisha kwamba huenda kukawa na changamoto ya kuhimili uhai wake ziwani,” aongeza.

Lakini kulingana na Bw Lumbasi, kwa sasa hawana budi ila kujaribu kwani huenda mradi huu ukawa matumaini yaliyosalia, endapo tunataka kurejesha fahari ya Ziwa Nakuru.

“Kwa sasa, tunasalia na chaguzi mbili; kupoteza matumaini na kukubali hali ya sasa ya ziwa hili, au kuimarisha viwango vya PH vya maji ya ziwa hili kwa kumwaga aina ya chumvi kama vile sodium bicarbonate, au chloride majini.”

Bw Lumbasi asema, mbali na kuwa ni ghali mno, huenda shughuli hii ikasababisha madhara zaidi majini, katika siku zijazo.

“Kwa mfano, ikiwa viwango vya maji vitapungua katika siku za usoni, huenda ziwa hili likawa na chumvi nyingi kiwango cha kukosa kuweza kuhimi uhai wowote,” aongeza.