Habari za Kaunti

Serikali yafufua ujenzi wa bwawa la Itare

May 21st, 2024 2 min read

NA JOHN NJOROGE

MRADI uliokwama wa Bwawa la Itare eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru utafufuliwa na ujenzi wake kukamilika kufikia mwaka 2028, msemaji wa serikali Isaac Mwaura amesema.

Akizungumza katika ziara ya kukagua eneo hilo Jumatatu jioni, Dkt Mwaura alisema yote yamepangwa kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

“Serikali ya Kenya imekamilisha mahitaji yote muhimu ili kuhakikisha mradi unaendelea kama ilivyopangwa. Tuna fedha zote za kukamilisha mradi huo katika kipindi cha miaka minne kwa gharama ya zaidi ya Sh40 bilioni kutoka Sh35 bilioni kufuatia kuongezeka kwa bei za vifaa vya ujenzi,” alisema Dkt Mwaura, akiongeza kuwa mradi huo ambao uko kwenye ekari 364, unafadhiliwa kikamilifu na serikali ya Italia.

Mradi huo utaunda nafasi za kazi kwa zaidi ya watu 10,000 mwishoni mwa ujenzi.

Baadhi ya mashine katika mradi uliokwama wa Bwawa la Itare wa mabilioni ya pesa huko Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru mnamo Mei 20, 2024. PICHA | JOHN NJOROGE

Alibainisha kuwa malimbikizo ambayo hayajalipwa kwa watu waliowahi kufanya kazi kwenye mradi huo, ikiwa ni pamoja na fidia ya wachache ambao hawakuwa wamelipwa, nayo yatalipwa kikamilifu.

“Wakazi wa Kaunti ya Nakuru watapata lita 120 milioni za maji safi kwa siku mradi huu ukikamilika. Kwa sasa, wakazi wa Nakuru wanapata maji kwa mgao, ama mara mbili au tatu kwa wiki, lakini hii itafikia kikomo mradi utakapokamilika ifikapo mwaka 2028,” akaeleza msemaji huyo.

Alifichua kuwa wakazi wa Nakuru hutegemea maji ya visima 40 ambavyo havitoshi kuhudumia wote kwani idadi ya watu imeongezeka na eneo hilo ambalo hadhi imeinuliwa hadi jiji.

Bi Gladice Cherotich, ambaye ni mkazi, alisema wametamani maji kwa miaka mingi, akiongeza kuwa sasa wana matumaini ya kupata maji ya kutosha kutoka kwa bwawa hilo.

Mkazi huyo alitoa wito kwa serikali kuwapa makazi mbadala wale waliofurushwa kutoka eneo hilo wakati bwawa hilo lilikuwa likijengwa.

Msemaji wa Serikali Dkt Isaac Mwaura akiandamana na viongozi wengine katika ziara ya kukagua mradi uliokwama wa Bwawa la Itare eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru mnamo Mei 20, 2024. PICHA | JOHN NJOROGE

Dkt Mwaura aliandamana na Afisa Mkuu wa Maji wa Kaunti ya Nakuru Bi Margaret Kinyanjui na Waziri wa Kilimo wa Kaunti ya Nakuru Leonard Borr miongoni mwa viongozi wengine kutoka kaunti hiyo.

Dkt Mwaura yuko katika Kaunti ya Nakuru kwa siku tano kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ufufuaji wa kilimo cha pareto.

Msemaji wa Serikali Dkt Isaac Mwaura akihutubu alipoandamana na viongozi wengine katika ziara ya kukagua mradi uliokwama wa Bwawa la Itare eneo la Kuresoi Kaskazini, Kaunti ya Nakuru mnamo Mei 20, 2024. PICHA | JOHN NJOROGE