Habari za Kitaifa

Tofauti kati ya Ruto na Gachagua zaendelea kudhihirika


TOFAUTI za kihisia kati ya Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua ziliendelea kuanikwa Jumapili, Juni 30, 2024, walipokinzana kuhusu suala nyeti linalohusu usalama wa nchi.

Kwenye mahojiano na wahariri wa mashirika makuu ya habari nchini katika Ikulu ya Nairobi Jumapili usiku, Juni 30, 2024, Rais Ruto alikana madai ya Bw Gachagua kwamba Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) lilifeli kutoa habari za kutosha kwake na vikosi vya usalama kabla maandamano ya vijana kupinga Mswada wa Fedha wa 2024.

Dkt Ruto alisema kulikuwa na habari tosha za kijasusi kwamba wahalifu walikuwa wakipanga kuingilia maandamano ya amani ya Jumanne, Juni 25, 2024.

“Hii ndio maana tulijiandaa kukabiliana na hali hiyo. Endapo hatungejiandaa tungekuwa tukitoa idadi tofauti ya waliokufa,” Dkt Ruto akasema.

“Wahalifu hao, walikuwa wamelenga kulemaza kabisa asasi muhimu za serikali. Hii ndio maana walipovamia majengo ya bunge walifululiza moja kwamba hadi stoo ya silaha na katika kaburi la Jomo Kenyatta,” akaongeza.

Baada ya maandamano hayo yaliyopelekea vifo vya idadi ambayo haijajulikana, Bw Gachagua alielekeza lawama kwa Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji kwa kile alichodai ni kufeli kutoa habari za kijasusi kwa Rais Ruto kuhusu maandamano ya kupinga mswada huo tata.

Akiongea mjini Mombasa, Naibu Rais alimtaka Bw Haji kujiuzulu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

“Haji anafaa kujiuzulu kwa kutomwarifu Rais hisia za Wakenya kuhusu Mswada wa Fedha na kunyamaza wakati wahalifu fulani walikuwa wakipanga kushambulia majengo muhimu ya serikali kama vile bunge. Amemuaibisha Rais na serikali na hivyo hana budi ila kujiuzulu,” Bw Gachagua akasema.

Wakati huo huo, saa chache kabla ya Rais Ruto kufanya mahojiano na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi, Bw Gachagua alikuwa katika kaunti ya Bomet akikiri kuwa kumekuwa na tofauti kati yake na bosi wake.

Hata hivyo, aliwahakikishia Wakenya kwamba watasuluhisha tofauti zao ili waendelee kusukuma gurudumu la kuliongoza taifa hili vizuri.

“Sina shaka kwamba Rais na mimi ni marafiki wa dhati na hatuwezi kuruhusu mtu yeyote kuja katikati yetu. Tutasuluhisha masuala yote ibuka kati yetu. Tutatoa wito kwa viongozi kushusha joto la kisiasa,” Bw Gachagua akasema.

Alikuwa akihutubu katika Kanisa la Deliverance mjini Kaplong, Bomet wakati wa ibada ya Jumapili na harambee ya kuchanga pesa kuendeleza kanisa hilo.