Habari za Kitaifa

Ubalozi wa Kenya London wadaiwa deni la Sh535m

May 22nd, 2024 1 min read

NA HILARY KIMUYU

UBALOZI wa Kenya jijini London, Uingereza unadaiwa Sh535 milioni za usafiri.

Ada na faini hizo hazijalipwa kwa muongo mmoja, na sasa London inapanga kuwasilisha suala hilo katika mahakama za kimataifa.

Kenya, kulingana na takwimu zilizochapishwa na TfL inayosimamia sekta ya uchukuzi London, ikiwa ni pamoja usafiri kupitia mabasi, magari na baiskeli zilifichua kuwa Kenya inadaiwa Sh530 milioni.

“Baadhi ya madeni hayo hulipwa ila kuna wale wanaokaidi sheria hiyo,” TfL ilisema katika taarifa.

“Tutaendelea kufuatilia ada zote za malipo ya msongamano wa magari ambazo hazijalipwa na notisi zinazohusiana na malipo ya adhabu, na tunashinikiza suala hilo kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.”

Ada hiyo iliyozinduliwa mwaka wa 2003 inahusisha ada ya kila siku ya Sh2,400 kwa kuendesha gari katikati mwa jiji la London kati ya saa moja asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni na saa kumi na mbili jioni wikendi.

Takwimu zilizochapishwa na TfL pia zilionyesha Amerika ilikuwa inaongoza kwa angalau 2 bilioni ikifuatiwa na ubalozi wa Japan, ambao unadaiwa Sh1.6 bilioni na India inayodaiwa Sh1.4 bilioni.