Habari Mseto

Wakili azikwa mkewe akikabili shtaka la mauaji

March 18th, 2019 2 min read

Na FLORAH KOECH

HUZUNI ilitanda Jumamosi katika kijiji cha Boritwo, eneo la Kalabata, Baringo Kaskazini wakati wa mazishi ya wakili aliyeuawa Robert Chesang.

Bw Chesang, 45, aliuawa kwa kupigwa risasi Februari 17 nyumbani kwake katika mtaa wa Moke Gardens, eneo la Lukenya, Kaunti ya Machakos mchana peupe na wanaume wawili waliotoroka mara baada ya kumuua.

Mkewe, Bi Pauline Omungala, ambaye ni hakimu katika Kaunti ya Nyeri, hakuhudhuria mazishi hayo kwani alikamatwa pamoja na washukiwa wengine watatu kwa mauaji hayo.

Watoto wake wawili pia hawakuwepo mazishini.

Wakili huyo wa Mahakama Kuu aliombolezwa kama mwanamume aliyekuwa na bidii, mkarimu na mwenye maadili mema, ambaye hakupenda kugombana na mtu yeyote kwa sababu yoyote ile.

Kakake, Daniel Chesang, alisema marehemu hakustahili kufa kwa njia hiyo na akataka waliomuua waadhibiwe kisheria.

“Natamani ningejua kwa nini kaka yetu alifariki kifo cha kikatili namna hii. Natamani tungeambiwa kama alikuwa na deni la mtu yeyote, kwani tungelipa madeni hayo ili kuokoa maisha yake. Hatutapumzika hadi tuhakikishe waliohusika na ukatili huu wameadhibiwa,” akasema Bw Chesang.

Bw Brian Kulei, ambaye alikuwa mwanafunzi wa marehemu katika Chuo Kikuu cha Kenyatta bewa la Parklands, alimsifu wakili huyo kama mwalimu ambaye alikuwa amejitolea katika kazi yake kila mara.

Wakili Vincent Kiptoon naye alisema marehemu alikuwa mtu aliyependa kusoma sana na kufanya utafiti.

“Chesang alikuwa rafiki yangu wa dhati na alikuwa akinipigia simu kila mara alipokuwa katika Mahakama ya Milimani. Niliposikia kwamba wakili mwenye jina sawa na lake amepigwa risasi akafariki, nilimwomba Mungu isiwe ni yeye. Hatutapumzika hadi tuhakikishe kuwa yeyote aliyehusika katika mauaji haya ameadhibiwa vikali,” akasema Bw Kiptoon.

Mbunge wa Baringo Kaskazini, Bw William Cheptumo alidai kifo hicho kilikuwa kimepangwa na watu waliyetaka kumwangamiza kwa njia yoyote ile.

“Ninatoa wito kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) ihakikishe wamefanya uchunguzi wa kina kuhusu mauaji haya. Hatutaki iwe baada ya muda mchache tutasikia washukiwa wameachiliwa huru kwa madai kuwa hapakuwa na ushahidi,” akasema Bw Cheptumo.