Habari za Kitaifa

Wasiwasi wagubika mawaziri kufuatia ripoti za uwezekano wa shoka kuanguka


WASIWASI umetanda katika Baraza la Mawaziri huku Rais William Ruto akiripotiwa kupanga mabadiliko katika juhudi za kuzima maandamano yanayoendelea nchini dhidi ya serikali.

Imeibuka kuwa, Rais Ruto anatazamiwa kuwafuta kazi baadhi ya Mawaziri na Makatibu – ambao wamewahi kuhusishwa na madai ya ufisadi.

Mawaziri na makatibu wasiofanya kazi vyema wako katika hatari ya kuangushiwa shoka Rais akijaribu kutuliza waandamanaji ambao wamekuwa wakitaka ajiuzulu.

Baadhi ya Mawaziri pia wanaweza kupatiwa kazi nyingine, huku Rais akisemekana kushauriana kuona iwapo atawabadilisha.

“Baraza la Mawaziri nililo nalo labda wangefanya vyema zaidi na nitafanya uchunguzi kuona jinsi tutakavyosonga mbele,” Rais Ruto alisema katika mahojiano Jumapili.

Alipoulizwa iwapo atawatimua Mawaziri, Rais alisema “subiri” ishara kuwa ana mipango ya kuwatimua baadhi ya mawaziri wake, ambao wamechangia mzozo uliopo.

Kwa takriban miaka miwili ambayo amekuwa madarakani, kumekuwa na dhana kwamba Rais na viongozi wake wa juu wana jeuri na hawachelei kuonyesha ubaridhirifu wa wazi wa fedha kupitia mavazi na magari yao—na mara nyingi kuchanga kiasi kikubwa cha fedha.

Taifa Leo imebaini kuwa, shoka linaweza kutua Bungeni, na kuathiri wenyeviti wa kamati na wale walio katika uongozi wa Bunge.

Waandamanaji wiki jana walivamia Bunge kuonyesha kutokuwa na imani na wabunge waliopiga kura kuunga Mswada wa Fedha wa 2024 maandamano yakiendelea.

Kulingana na duru za serikali, uhusiano baridi kati ya Rais Ruto na naibu wake, Bw Rigathi Gachagua, unazua utata mwingine wa kisiasa.

Duru zilisema Rais yuko tayari kufanya mabadiliko hayo wiki hii, lakini kuna hofu kwamba, mabadiliko hayo yanaweza kupanua mpasuko kati ya viongozi hao wawili kwa kuwa baadhi ya washirika wa Bw Gachugua huenda wakaathiriwa katika mabadiliko hayo.

“Ni wazi kuwa Rais yuko tayari kufanya mabadiliko fulani katika serikali yake. Itakuwa vigumu kwangu kuzungumzia jambo hili waziwazi, lakini ndio ukweli,” alisema afisa mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Haikuweza kufahamika mara moja ikiwa Rais atashauriana na Bw Gachagua katika kufanya mabadiliko hayo huku ikiibuka kuwa Naibu Rais hajafika Ikulu kwa muda wa wiki mbili zilizopita.

Alionekana mara ya mwisho Ikulu wakati wa mkutano wa Kikundi cha Wabunge wa Kenya Kwanza ambao ulifanyika Juni 18.

Washirika wa Rais Ruto Jumatano walisusia mazishi ya dada mkubwa wa Bw Gachagua Leah Wangari Muriuki, ambaye alizikwa Nanyuki.

Linturi pekee awa waziri aliyehudhuria mazishi ya dadake Gachagua

Katika Baraza la Mawaziri, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi pekee ndiye aliyehudhuria.

Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed hakujibu maswali yetu kuhusu msukosuko katika Baraza la Mawaziri.

Bi Njeri Rugene, mkuu wa Huduma ya Mawasiliano wa Naibu Rais, alisema afisi hiyo haikuwa na habari kuhusu mabadiliko yaliyopangwa katika Baraza la Mawaziri.

Wito wa kutaka mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ulitawala hoja kuhusu Hali ya Taifa katika Seneti jana wakati baadhi ya wanachama wa UDA walipomuomba Rais waziwazi kuwatimua baadhi ya mawaziri.

Kiranja wa Wengi katika Seneti Boni Khalwale alimtaka Rais kuwatimua mawaziri wazembe ili kutuliza waandamanaji.

“Mheshimiwa Rais, vunja Baraza la Mawaziri na uliundie upya. Ondoa afisi nje ya Katiba kama vile mawaziri wasaidizi na Mkuu wa Mawaziri, ofisi za wake wa kwanza na washauri,” akasema Bw Khalwale.

Pia, alitoa wito wa kufanyiwa marekebisho upya idara za usalama kwa kumfuta kazi Inspekta Jenerali Japhet Koome.

“Tuna DPP (Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma) ambaye hukaa kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa kupanga lugha na sheria ya kutumia… Acha wahalifu ambao wameiba mali wapitie utaratibu unaostahili. Kama angefanya kazi, baadhi ya mawaziri hawangekuwepo. Wengine wapo kwa sababu Bunge fisadi liliwaruhusu na DPP alifuatilia kwa kufuta kesi zao,” alisema ndani ya Bunge.

Vile vile, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alitoa wito kwa uteuzi wote wa umma uliofanywa tangu Septemba 2023 uchunguzwe upya, akisema baadhi ya afisi zilizoundwa hazifai kuwepo.