Afya na Jamii

Wauguzi wakimbilia kazi ughaibuni wakiacha Kenya kwa balaa

May 15th, 2024 3 min read

NA MAUREEN ONGALA

WADAU katika sekta ya afya wameingiwa na wasiwasi baada ya kugundulika kwamba hata wauguzi wa hospitali za mashinani wanatafuta ajira ughaibuni.

Katika siku za hivi punde, kumeshuhudiwa idadi kubwa ya wauguzi wanaotafuta ajira katika mataifa ya nje huku serikali ya kitaifa ikiunga mkono harakati hizo zao.

Kwa miezi michache ambayo imepita, wauguzi wengi wanayoyomea nchi za bara Ulaya, Amerika, na katika mataifa ya Mashariki ya Kati.

Kulingana na Muungano wa Wauguzi na Wakunga katika Kaunti ya Kilifi, hali hiyo ilikuwa ya kawaida miongoni mwa madaktari na wauguzi waliokuwa wakifanya kazi maeneo ya mijini lakini hali ni tofauti ambapo hata wale walio katika vituo vya afya vya mashambani wanasafiri kufanya kazi nje ya nchi.

Hayo yalijadiliwa Jumatatu katika Hospitali ya Rufaa ya Kilifi wakati wa maadhimisho ya wiki ya Wauguzi na Wakunga.

“Baada ya mgomo wa wauguzi mwaka 2017, wauguzi wengi walivunjika moyo na kudhoofika kifedha na wengi wakaanza kuhamia ughaibuni kutafuta riziki… ”

“Miaka ya nyuma, ni madaktari na wauguzi wa jijini Nairobi waliopendelea kuhamia ng’ambo, lakini tunavyozungumza sasa wenzetu wengi katika vituo vya mashinani wako katika harakati za kuhamia huko, huku wengi wakiwa tayari wameenda,” Mratibu wa Afya ya Uzazi katika Kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti akasema.

Bw Miriti anasema serikali–ya kitaifa na za kaunti–haijajitolea kikamilifu kukabili suala hili la uhaba wa wauguzi, hali inayozua hofu.

Anaongeza kwamba wauguzi wengi, kwao fursa ya kufanya kazi nje ya nchi inavutia kwa sababu ya mazingira bora ya kazi na mishahara wanayotarajia huko ikilinganishwa na hapa Kenya.

Lakini huku kuyoyomea kwa mataifa ya kigeni kunaacha pengo kubwa kwa sababu raia maskini huwa wamekosa kabisa mhudumu muhimu wa afya katika zahanati za mashinani ambazo nyingi husimamiwa na wauguzi.

“Hatujapewa fursa ifaayo katika mfumo wa huduma za afya. Serikali imepuuza suala la mishahara kwa wauguzi ambalo ni muhimu sana. Utakuta afisa wa kliniki anayefanya kazi na muuguzi katika zahanati anapata mshahara mkubwa zaidi huku muuguzi akitaabika,” akaongeza.

Kulingana na Bw Miriti, wauguzi wastaafu wamehisi hatari inayokabili sekta ya afya nchini.

Mratibu wa Afya ya Uzazi katika Kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti akihutubia wanahabari. PICHA | MAUREEN ONGALA

Kwa sasa kaunti ya Kilifi ina takriban wauguzi 760, huku duru zikisema kuwa baadhi yao wako katika harakati za kutafuta kazi ughaibuni.

Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Afya ya Familia katika Kaunti ya Kilifi, Bi Jesca Deche, anasema kuwa kuhama kwa wauguzi hao kumeathiri pakubwa utoaji wa huduma mashinani.

“Tunakabiliwa na uhaba wa wauguzi katika kaunti yetu. Baadhi walistaafu, wengine waliaga dunia, huku wengine wakiwa wameyoyomea nje ya nchi kwa sababu ya mishahara duni ya wauguzi nchini Kenya,” akasema Bi Deche.

Bi Deche anasema Bodi ya Utumishi wa Umma ya Kaunti ya Kilifi haijawaajiri wauguzi kwa zaidi ya miaka mitano licha ya uhaba ulioko.

“Wauguzi wengi ambao wamekuwepo ndani ya kipindi hicho wamekwenda nje ya nchi, hali inayoathiri sana utoaji wa huduma katika zahanati na kutulazimu kuajiri wauguzi kwa mkataba katika hospitali za rufaa,” akasema.

Bi Deche anasema ubora wa huduma inayotolewa na wauguzi wanaopata kazi siku hizi ni ya kiwango cha chini kwa sababu huwa hawana mtu mzoefu wa kuwaelekeza.

Anasema huduma ya afya ya uzazi ndio inayoathirika zaidi.

Licha ya kwamba madaktari wamerudi kazini baada ya mgomo wao uliodumu kwa siku 56, Bi Deche anasema ipo haja ya wauguzi kutambuliwa kote nchini kwa kuwa walifanya kazi nzuri ya kusimamia hospitali kipindi hicho kigumu.

“Ni tatizo kubwa na lisipotatuliwa, ni bomu linaloweza kulipuka wakati wowote… hivyo serikali izibe pengo lililopo,” akasema.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wauguzi (KNUN) tawi la Kilifi Bi Juliana Nyevu anasema zaidi ya wauguzi 450 wanasubiri kupandishwa cheo na Bodi ya Huduma za Umma katika Kaunti.

Bi Nyevu anasema wauguzi hao waliwasilisha barua zao kwa bodi hiyo.

Mkurugenzi wa Afya wa Kaunti ya Kilifi Dkt Hassan Leli anasema idara hiyo inashughulikia malalamishi ya wauguzi.

“Mfanyakazi yeyote husubiri malipo baada ya kazi na ndiposa tunafanya kazi bila kuchoka kuhakikisha wale wote wanaostahili kupandishwa vyeo wanapata na pia tunawapa hamasisho,” akasema Dkt Leli.

Wauguzi na wakunga wakiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kilifi mnamo Mei 13, 2024. PICHA | MAUREEN ONGALA