Habari za Kaunti

Wakazi washauriwa kujenga kwa mpango kuepuka kubomolewa nyumba

May 18th, 2024 2 min read

NA MAUREEN ONGALA

MWENYEKITI wa kamati ya mipangilio ya miji katika Bunge la Kaunti ya Kilifi amewashauri wenyeji na wakazi kujenga nyumba zao kwa mpango kuepuka hasara ya kufurushwa na kubomolewa makazi.

Bw Raymond Katana, ambaye ni mwakilishi wadi ya Sokoni, amewataka wakazi kuhusisha idara husika wakati wa ujenzi huo kama njia ya kujiepusha na hasara ya nyumba zao kuvunjwa ili kupisha miradi ya serikali kutekelezwa.

Akizungumza mjini Kilifi, Bw Katana alisema wakazi wengi wamekuwa wakipata hasara kubwa baada ya nyumba zao kubomolewa kutokana na majengo mengi kujengwa sehemu zisizo sahihi.

Bw Katana alieleza kuwa wengi wamekuwa wakijenga sehemu za barabarani, hali anayodai kuwa itawalazimu kuvunja majengo hayo ili kupisha miradi ya maendeleo kufanyika.

“Natoa onyo kwa wakazi wa Kilifi wasijenge katika sehemu za barabara kwa sababu wakati ukifika wa ujenzi wa barabara, mwanakandarasi atavunja nyumba hizo mwathiriwa akibaki kupiga kelele,” akasema Bw Katana.

Mwenyekiti huyo aliwashauri wote walio na mipango ya kuendeleza ujenzi mijini, kuhakikisha kuwa wanatembelea ofisi za mipangilio ya miji ili kuelezwa iwapo sehemu wanazonuia kuendeleza ujenzi ni sahihi au la.

Aidha, alitoa onyo kali kwa wote wanaojenga nyumba zao kiholela, akisistiza kuwa wanahatarisha maisha yao kwani majanga kama vile mafuriko yanapotokea, yanaweza kuwasababishia maafa makubwa.

“Ni lazima maafisa husika wahakikishe kuwa mahali panapojengwa mijengo ni salama, waangalie kama ni njia ya maji–panasimama maji au la–ili wakazi wasije wakasombwa na maji na kuanza kulalamika,” akasema.

Aliongeza kusema kuwa biashara inatarajiwa kuimarika mjini Kilifi kufuatia mradi wa ujenzi wa soko la wafanyabiashara wadogowadogo kuzinduliwa rasmi.

Soko hilo linalojengwa kwa awamu litakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya wafanyabiashara 150 ambao kwa sasa wanafanyia biashara zao kando ya barabara mjini humo baada ya vibanda vyao kubomolewa tangu Machi 2024.

Ujenzi wa soko hilo unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh12 milioni na kuchukua muda wa miezi sita kukamilika unalenga kuweka mazingira bora ya kuendeleza biashara.

Bw Mwaro alisema katika awamu ya kwanza, kutajengwa vibanda 54 huku nje ya soko hilo kukiwekwa makontena ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wote wanapata nafasi.

Bw Benjamin Musembi ambaye ni mwakilishi wa wafanyabiashara wadogowadogo katika barabara ya Absa hadi Rubis mjini Kilifi alieleza kuwa soko hilo litawasaidia kujiimarisha tena kiuchumi baada ya wengi kufilisika kutokana na kuvunjwa kwa vibanda vyao.

[email protected]