Habari Mseto

Afisa wa ngazi za juu NIS ajiua kwa kujipiga risasi kichwani

June 5th, 2024 1 min read

Na STEVE OTIENO

AFISA wa ngazi za juu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) amejiua kwa kujipiga risasi kichwani nyumbani kwake mtaani Kilimani, Nairobi.

Rekodi za polisi zinaonyesha kwamba mwendazake, aliyetambuliwa kama Tom Mboya Adala alikuwa naibu mkurugenzi katika makao makuu ya NIS yaliyoko Ruaraka.

Aliyeripoti kisa hicho katika Kituo cha Polisi cha Kilimani ambaye ni mpwa wake, Francis Oduor, aliambia polisi kwamba mjombake alijipiga risasi upande wa kulia wa kichwa na risasi ikatokea upande wa kushoto.

Oduor aliambia maafisa kwamba alimuona mjombake mara ya mwisho Juni 3, 2024 kama saa nne usiku alipoenda kulala kwenye chumba chake.

Hata hivyo, alishuku kulikuwa na jambo baya wakati siku iliyofuata kufikia saa tatau asubuhi, hakuwa ameonekana.

“Mtoaji taarifa alienda kwenye orofa ya juu kumuangalia katika chumba chake lakini hakuwepo. Akamuuliza mlinzi ambaye alikuwa kwenye lango nje iwapo mwendazake alikuwa ameondoka nyumbani, akamwambia hajatoka,” sehemu ya ripoti inasema.

Hili lilifanya mpwa huyo kuzunguka nyumba nzima akimtafuta mjombake na ni hapo alimkuta kwenye nyumba ya wajakazi akiwa chini tayari amekufa.

Hapa ndipo alipigia simu jamaa wa familia na kujulisha polisi mara moja. Eneo la mkasa lilitembelewa na Naibu Kamanda wa kaunti ndogo, Kilimani, Afisa wa Upelelezi, Afisa Mkuu wa Kilimani na maafisa wa ngazi za juu wa NIS.

Bastola aina ya glock 19 ilipatikana ikiwa na ganda moja la risasi iliyotumika. Polisi walipata pia barua ya kuelezea sababu za kujitoa uhai iliyokuwa imewekwa kitandani katika chumba cha kulala cha marehemu.

“Mwendazake anasemekana alikuwa akikabiliana na msongo wa mawazo kwa muda. Hatua hitajika zimechukuliwa na mwili umepelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee,” ikasema ripoti.

Uchunguzi umeanzishwa.