Habari Mseto

Gachagua asafiri kwa ndege ya KQ kuhudhuria kongamano Mombasa

June 11th, 2024 1 min read

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua Jumanne aliamua kuabiri ndege ya Shirika la Kenya Airways (KQ) katika kile kinachoonekana kulenga kuonyesha kuwa kweli amezuiwa kutumia helikopta za kijeshi.

Aidha, anaonekana kutuma ujumbe kuwa yeye sio mmojawapo wa maafisa wa serikali wanaoshiriki ubadhirifu wa pesa za umma kwa kutumia ndege zilizokodishwa.

Kwenye picha zilizozungushwa mitandaoni Jumanne, Bw Gachagua anaonekana akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) akiwa amebeba mkoba wake tayari kuabiri ndege ya KQ kama abiria wa kawaida.

Katika picha nyingine anaonekana akiingia ndani ya ndege akiwa anabururu mkoba huo alielekezwa na wahudumu wa shirika la KQ.

Duru za afisi ya Naibu Rais ziliambia Taifa Leo kwamba Bw Gachagua alikuwa akielekea Mombasa kuongoza ufunguzi rasmi wa Kongamano la Kisayansi la Kimataifa la Chama cha Wanafamasia wa Kenya.

Shughuli hiyo itafanyika Jumatano katika mkahawa wa Sarova Whitesands jijini Mombasa.

Katika siku za hivi karibuni, wandani wa Bw Gachagua wakiongozwa na Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga wamekuwa wakilalamikia kile wanachokitaja kama kudhalilishwa kwa Bw Gachagua kwa kunyimwa nafasi ya kutumia ndege za kijeshi.

Mnamo Jumapili Bw Gachagua pia alionyesha hali hiyo alipodai kuwasili kuchelewa katika kongamano la Dhehebu la Akorino mjini Nakuru kutokana na kile alichokitaja kama “changamoto ya usafiri”

Majuma mawili yaliyopita Waziri wa Ulinzi Aden Duale alipiga marufuku wanasiasa, isipokuwa Rais, kutumia helikopta na vyombo vingine vya usafiri vya Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF).