Michezo

Haaland adidimiza matumaini ya Arsenal kwa kusaidia Man City kukomoa Spurs 2-0

May 15th, 2024 1 min read

Na MWANGI MUIRURI

MABAO ya Erling Braut Haaland wa Manchester City dhidi ya Tottenham Hotspur katika dakika za 51 na 90+1 yalivunja nyoyo za mashabiki wa Arsenal kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumanne usiku.

Timu hiyo ya Spurs ndio ilikuwa tegemeo kuu la Arsenal kutwaa taji la EPL msimu huu wa 2023/24 lakini kwa sasa mambo ni kama yameharibika kabisa.

Huku Arsenal na Man City zikibakisha mechi moja moja ndio msimu utamatike, hali ni kwamba ni kama msimu umeponyoka The Gunners.

Kwa sasa, Man City inaongoza jedwali kwa pointi 88 huku Arsenal ikiwa ya pili kwa pointi 86 kila moja ya timu hizi mbili ikibakisha mechi moja pekee.

Arsenal sasa itatarajia kwamba West Ham United iwe tegemeo la mwisho la kusimamisha Man City huku nayo ikiomba ikomoe Everton katika mechi ya mwisho.

Hadi sasa, Arsenal ikiwa na ubora wa bao moja ingetarajia Man City itoke sare yoyote ikiwa sio kupigwa ndio hesabu yake ya kutwaa taji iwe na maana.

Mtanange huo wa Man City na Spurs ulikuwa unafuatiliwa kwa karibu na wafuasi wa Arsenal na kila dakika ya kuanzia 51 wakati bao hilo la kwanza lilifungwa ikawa ni hali ya mahangaiko na masikitiko.

Kuzawadiwa penalti katika dakika ya 90+1 nusura kuwafanye wafuasi wa Arsenal waangue kilio wakiona matumaini yao yakiangamizwa na kuwekwa kwa jeneza huku mechi ya mwisho ikiwa sasa ndio ya kuamua hatima ya timu hizo mbili.

Tayari, Liverpool imejihakikishia nafasi ya tatu nayo Aston Villa ikiwa na uhakika wa kumaliza katika nafasi ya nne.

Timu za Luton, Burnley na Sheffield town tayari zimetimuliwa kutoka EPL kwa kumaliza katika nafasi tatu za mwisho katika ligi hiyo ya timu 20.

Nyingine tatu zitapandishwa ngazi kutoka ligi la daraja ya pili ya Championship.