Michezo

Harambee Stars watua Malawi na kuzamia mazoezi mara moja

June 4th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

HARAMBEE Stars leo itaanza mazoezi kabambe nchini Malawi ikijiandaa kutifua vumbi kali katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Burundi na mabingwa wa Afrika Cote d’Ivoire.

Kenya itapambana na Burundi katika mechi ya Kundi F Ijumaa hii kabla ya kuvaana na Cote d’ivoire (Ivory Coast) Jumanne ijayo.
Mechi hizo zote zitachezwa kwenye uwanja wa Mbingu Mutharika, jijini Lilongwe.

Mechi zote mbili zitaanza saa 10 jioni mnamo Ijumaa na Jumanne. Kenya iliahiri kusakata mechi hizo mbili ugenini kutokana na ukarabati ambao unaendelezwa kwenye nyuga za Nyayo na Kasarani.

Kikosi cha vijana 25 jana kiliondoka nchini hapo jana saa 12 asubuhi na kufika Lilongwe saa mbili asubuhi.

Vijana walipumzika na kufikia jana jioni, afisa mmoja aliyesafiri na timu hiyo alisema kuwa bado walikuwa wakisaka uwanja wa kufanyia mazoezi.

Hata hivyo, kulikuwa na mabadiliko katika kikosi kilichosafiri baada ya kiungo Eric Johana anayesakatia UTA Arad kuangushiwa shoka na nafasi yake ikachukuliwa na winga wa AFC Leopards Clifton Miheso.

Duru zinaarifu Johana aliingia mitini baada ya wachezaji kuruhusiwa kuenda kupumzika mnamo Ijumaa na akakosa kurejea kambini mnamo Jumamosi jioni.

“Alizima simu na huenda alikuwa ameenda kuburudika au kushiriki shughuli zake tu za kawaida. Ni vyema angesema kama hataki kuchezea timu ya taifa badala ya kukataa kuchukua simu,” duru zikaarifu.

Kuelekea mechi hiyo, beki Tobias Knost wa SV Verl ya Ujerumani amesema kuwa itakuwa fahari kubwa kwake kuchezea Harambee Stars na kipindi ambacho amefanya mazoezi na timu hiyo amejifunza mengi.

Knost, 24 ambaye alichezea Ujerumani Under 18, atakuwa akisakatia Harambee Stars kwa mara ya kwanza iwapo atawajibishwa dhidi ya Burundi au Cote d’ivoire.

“Kuchezea kikosi cha Harambee Stars ni fahari kuu na ni ndoto ambayo imetimia. Pia ni wakati wa kuwakilisha nchi yangu na nimefurahi sana,” wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

“Nataka nijitume sana na kuthibitisha benchi ya kiufundi kuwa hawakukosea kwa kunijumuisha kikosini. Tutakuwa tukicheza dhidi ya wapinzani wakali na najua tutashinda,” akaongeza Knost.