Habari za Kitaifa

Madaraka Dei: Wito wa kukabili muguka watolewa

June 1st, 2024 2 min read

JURGEN NAMBEKA Na MAUREEN ONGALA

SHEREHE za 61 za Madaraka Dei katika Kaunti ya Mombasa zilizofanyika bustani ya Mama Ngina zilisheheni siasa za vita dhidi ya muguka viongozi wa eneo la Pwani wakilaanu mmea huo.

Wakiongozwa na gavana wa kaunti hiyo na wabunge waliohudhuria sherehe hizo, walimtaka Rais William Ruto kuwapa nafasi ya kukutana nao na kujadili madhara ya mumea waliosisitiza ni dawa ya kulevya.

Akizungumza katika sherehe hizo, mbunge wa Kisauni Bw Rashid Bedzimba aliwaomba wakazi kuunga mkono vita hivyo akidai kuwa kwa kukosa wanunuzi huenda wafanyabiashara hao watabadili mawazo yao.

“Tulijinyakulia madaraka ili tupambane na mambo ambayo yalikuwa yakituhangaisha humu nchini. Kwa sasa nyinyi mumeona madhara ya muguka na mihadarati mingine. Ndiposa tumemuunga mkono Gavana Abdulswamad Nassir. Nataka wakazi mujizuie kununua muguka ili wao waone haina faida huku,” akasema Bw Bedzimba.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko alimtaka Rais Ruto kujitokeza na kukutana na viongozi wa Pwani, na kuomba Waziri wa Kilimo Mithika Linthuri kutohusika na vikao hivyo.

“Mheshimiwa Rais, sisi hatutaki kikao na Bw Linthuri. Yeye ana mambo mengi ya kushughulikia ikiwemo sakata ya mbolea feki. Kama ulivyokutana na wale viongozi wa kule muguka unatoka, kutana na sisi ili tukueleze madhara yake kwa jamii yetu,” akasema Bi Mboko.

Kwa mujibu wa mbunge huyo tayari athari zake zilikuwa zimeanza kuonekana kwa wanafunzi akisema amepokea ripoti za wanafunzi kupatikana na vifurushi vya muguka kwa kuwa inapatikana kwa wingi.

Kwingineko mbunge wa Ganze Kenneth Kazungu amesema kuwa vita dhidi ya muguka vitaendelea bila uoga.

Bw Kazungu alisema kuwa ni lazima rais na makamu wake wasikize sauti ya viongozi wa wapwani ambao wamesimama kidete kupigania jamii ambayo inaangamia kutokana na matumizi makubwa wa muguka.

Usemi wa mbunge huyo unawadia huku wakazi wa kaunti ya Kilifi wakiandamana kupinga biashara ya muguka kutokana na athari zake kwa vijana, wanawake na watoto.

Akizungumza katika shule ya msingi ya Bale wakati wa kuzindua rasmi ukarabati wa madarasa, Bw Kazungu alisema kuwa baada ya mkutano ya viongozi kutoka kaunti ya Embu wakiongozwa na gavana Cecily Mbarire, Rais Ruto hakuwahuhisha viongozi wa Pwani kabla ya maamuzi yake.

“Tunapoteza kizazi chetu ndio maana tunapinga muguka. Rais alichukua hatua bila kuhusisha viongozi wa Pwani na cha kushangaza ni kuwa alitenga Sh500 kuimarisha mmea wa muguka,” akasema Bw Kazungu.