Habari za Kitaifa

Magavana wa mhula wa kwanza wasalia bila miradi mipya miaka miwili tangu uchaguzi

Na ERIC MATARA July 4th, 2024 3 min read

LICHA ya kuwapa wapigakura ahadi nyingi, baadhi ya magavana wapya bado hawajaanzisha miradi mipya ya maendeleo zaidi ya mwaka mmoja tangu waingie mamlakani.

Magavana wengi wanatatizwa na gharama ya mishahara inayomeza zaidi ya nusu ya bajeti ya kaunti zao kila mwaka, madeni ambayo hayajalipwa, yakiwemo yaliyokuwa ya mabaraza ya miji na miradi iliyokwama ambayo walirithi kutoka kwa watangulizi wao.

Ufichuzi kuwa mgao wa mapato kwa kaunti utapunguzwa kutokana na kuondolewa kwa Mswada wa Fedha wa 2024, unaweza kutatiza hali ya kifedha katika kaunti na kuzima miradi ya maendeleo.

Kaunti zilikuwa zimetengewa Sh415 bilioni katika mwaka wa kifedha 2024/2025.

Kulingana na ripoti ya hivi punde ya Mdhibiti wa Bajeti Margaret Nyakang’o, iliyohusisha miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa fedha wa 2023/2024, zaidi ya magavana 30 hawajatekeleza miradi ya maana ya maendeleo huku kaunti tano pekee – Narok, Bomet, Uasin Gishu, Mandera, na Kitui zikifikia viwango vya juu vya utumiaji wa bajeti zao za maendeleo zilizoidhinishwa.

Ripoti hiyo inaonyesha Kaunti za Nairobi, Bungoma, Mombasa na Taita Taveta ndizo zilizo na viwango vya chini zaidi vya utumiaji wa bajeti kwa miradi ya maendeleo iliyoidhinishwa.

Ripoti hiyo inaonyesha rekodi ya maendeleo katika kaunti ya Bungoma ilikuwa asilimia 11.7, Jiji la Nairobi asilimia 9, Mombasa asilimia 7.7 na Taita Taveta kwa asilimia 7 mtawalia.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa Nairobi ilitumia Sh1.25bilioni pekee kwa maendeleo katika bajeti ya Sh11.35bilioni, Bungoma (Sh660 milioni) dhidi ya bajeti ya Sh4.48 bilioni, Mombasa (Sh369 milioni) dhidi ya bajeti ya Sh4.4 bilioni na Taita Taveta (Sh163 milioni) dhidi ya a bajeti ya Sh2.19 bilioni mtawalia kwa maendeleo.

Narok, Bomet, Uasin Gishu, Mandera na Kitui zinaongoza kwa kiwango cha juu cha miradi

“Jumla ya matumizi ya serikali za kaunti katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024 yalikuwa Sh274.08 bilioni, ambayo ni sawa na asilimia 48.5 ya jumla ya bajeti ya kila mwaka ya serikali za kaunti ya Sh564.53 bilioni,” ilisema ripoti.

Ripoti hiyo ilionyesha kwamba matumizi ya maendeleo ya serikali za kaunti katika miezi tisa ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2023/24 yalifikia Sh44.89 bilioni, na kufanya kiwango hicho kuwa asilimia 22.1.

Kaunti za Narok, Bomet, Uasin Gishu, Mandera na Kitui zilifikia viwango vya juu vya utumiaji wa bajeti zao za maendeleo zilizoidhinishwa kwa asilimia 54.4, 48.8, 41.5, 38 na 36.6 mtawalia.

Kaunti pia zimekuwa zikijikuna vichwa kulipa madeni.

Kwa mfano kaunti zililipa madeni ya Sh10.5 bilioni kufikia Desemba 2023.

Takriban kaunti 43 ziliripoti kutumia kati ya Sh17 milioni na Sh1.8 bilioni kila moja kulipa wafanyabiashara katika muda wa miezi sita.

Kufikia mwisho wa Desemba 2023, ripoti ya CoB ilionyesha kaunti zote 47 zilidaiwa Sh 156.3 bilioni.

“Uchambuzi wa madeni hayo unaonyesha kuwa Kaunti ya Jiji la Nairobi inadaiwa Sh107.04bilioni. Kaunti zingine zilizo na kiwango cha juu cha madeni ni Kiambu (Sh5.71 bilioni), Mombasa (Sh3.92 bilioni ), Machakos (Sh3.03 bilioni), Mandera (Sh2.3 bilioni) na Busia (Sh2.29bilioni),” Margaret Nyakang’o anaeleza kwenye ripoti hiyo.

Kufikia Desemba 2023, Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alikuwa ametumia Sh1.77 bilioni kulipa madeni.

Kaunti ya Turkana ilifuata kwa kulipa madeni ya kima cha Sh564.4milioni huku Tana River ikitumia Sh534.36 milioni katika muda wa miezi sita kulipa madeni.

Murang’a ilifunga orodha ya kaunti nne zilizotumia zaidi ya Sh 500 milioni, baada ya kutumia Sh512.78 milioni.

Kaunti nyingine nne, ambazo ni Embu, Migori, Nairobi na Kisumu, zilitumia kati ya Sh 400 milioni na Sh 490 milioni kila moja kulipa madeni.

Wengi wa magavana wapya pia wasingeweza kuanzisha miradi ya maana ya maendeleo kwa sababu ya miradi iliyokwama ambayo walipaswa kukamilisha.

Kwa mfano magavana wapya katika eneo la Bonde la Ufa wamekuwa wakikabiliana na jinamizi la kukamilisha miradi iliyokwama iliyogharimu zaidi ya Sh10 bilioni iliyoanzishwa na watangulizi wao.

Gavana wa Nakuru Susan Kihika, George Natembeya (Trans Nzoia) na mwenzake wa Uasin Gishu Jonathan Bii ni miongoni mwa waliorithi miradi kama hiyo kutoka kwa watangulizi wao, ambayo lazima wafadhili na kuharakisha kuikamilisha kabla ya kuzindua miradi yao wenyewe.

Wengine ni pamoja na; Benjamin Cheboi (Baringo) na Dkt Eric Mutai(Kericho).

Wakuu wa kaunti wanapaswa kukamilisha miradi hiyo hata wanapotafuta kuzindua miradi yao kuu.

Kaunti za Kisii, Garissa, Busia, Nyamira, Pokot Magharibi, Machakos, Embu, Nairobi na Wajir pia zimeorodheshwa na Mdhibiti wa Bajeti kwa kutumia zaidi ya asilimia 60ya mapato kwa mishahara.

Nyingine ni Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Laikipia,Trans Nzoia,Pokot Magharibi na Kiambu.