Michezo

Mashabiki waomba walipiwe nauli kwenda na Harambee Stars mechi ya Malawi

May 29th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

MASHABIKI wa soka nchini kupitia chama chao (KEFOFA) wamelilia serikali, Shirikisho la Soka Kenya (FKF) na wahisani wakitaka ufadhili kuisapoti Harambee Stars katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2026 nchini Malawi mwezi ujao.

Kenya itavaana na Burundi mnamo Juni 7 na kisha ichapane na mabingwa wa Afrika Cote d’Ivoire mnamo Juni 11 katika mechi za Kundi E uga wa Mbingu wa Mutharika.

Stars itacheza mechi zake za nyumbani ugenini kwa sababu nyuga za Nyayo na Kasarani zinakarabatiwa.

Kasarani itakuwa mwenyeji wa Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2027, huku Nyayo ikiandaa kipute cha CHAN baadaye mwaka huu.

Vijana wa kocha Engin Firat wanatarajiwa kuondoka nchini mnamo Juni 2 kuelekea Malawi kuwajibikia mechi hizo na tayari wameingia kambini kujitia makali.

Hapo jana, maafisa wa Kefofa walisema kuwa Malawi ni mbali na wakafichua kuwa wana basi moja ambalo wakipata ufadhili watasafiria kushangilia vijana wa taifa.

Afisa Mkuu Mtendaji Shem Okottah, hata hivyo, alisema wanalenga mabasi mengine saba ili mashabiki wawe wengi kwa mechi hizo mbili.

“Tunaomba wadhamini, washikadau na wapenzi wa soka wajitokeze kufadhili Kefofa ishangilie Harambee Stars Malawi. Safari hiyo ni ya mbali kupitia barabara na tunahitaji kutoka mapema,” akasema Okottah.

Wakati Kenya ilipokuwa ikishiriki AFCON mnamo 2019, wadhamini mbalimbali hasa kampuni za kamari, ziliwafadhili mashabiki kuelekea Cairo kuishangilia Stars.

Kupitia ufadhili wa Sportpesa, Kefofa iliwasafirisha mashabiki 70 kwa dimba la Afcon 2019. Kampuni nyingine nazo ziliandaa mashindano ya ubashiri na kuwazawidi mashabiki tikiti ya moja kwa moja.

“Tutakuwa Malawi kwa siku tano na hasa tunalenga kuwapa motisha vijana wetu ili waimarishe nafasi yao ya kufuzu. Sisi hatuthaminiwi na yeyote na huuza shati tao kwa Sh3,000 ili kuweka akiba,” akaongeza Okottah.

Kefofa inatambuliwa na serikali kupitia Wizara ya Michezo na imekwepo kwa zaidi ya miaka 60 na hasa hujihusisha na kujenga brandi ya timu ya taifa.

Wakati huo huo, Kenya Police jana ilidumisha ushindi wa 1-0 walioupata dhidi ya AFC Leopards katika mechi ya nusu-fainali ya MozzartBet Cup.

Mchuano huo jana ulichezwa kwa dakika 30 pekee baada ya kusimamishwa dakika ya 62 mnamo Jumapili kutokana na ghasia za mashabiki.