Dimba

Masihara yanayotishia Harambee Stars kugeuka kuwa ‘Harambee Stress’

June 8th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

TIMU ya taifa Harambee Stars inakabiliwa na kibarua kigumu katika kampeni za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026 baada ya Ijumaa kukabwa 1-1 na Burundi nchini Malawi.

Katika mechi hiyo iliyochezewa ugani Bingu, nguvu mpya Duke Abuya aliipa Stars uongozi dakika ya 72 baada ya kuandaliwa pasi na Austin Odhiambo.

Wawili hao walikuwa wameingia dakika ya 64 kuchukua nafasi za Timothy Ouma na winga Cliftone Miheso.

Hata hivyo, kosa la kitoto lililofanywa na Daniel Anyembe dakika ya 85 lilisaidia Burundi kusawazisha pia kupitia nguvu mpya Sudi Abdallah.

Harambee Stars sasa ina alama nne, sawa na Burundi katika Kundi F.

Mabingwa wa Afrika, Cote d’Ivoire (maarufu Ivory Coast), na Gabon ambao walikuwa wachuane baadaye Ijumaa wanaongoza na alama sita kila mmoja.

Gambia na Ushelisheli, ambao pia wapo kwenye kundi hilo, watakabana koo Jumamosi lakini bado timu hizo zilikuwa hazijajizolea alama zozote.

Kenya sasa inakabiliwa na mlima mkubwa wa kukwea Jumanne ijayo ikipambana na Ivory Coast katika uwanja huo huo wa Bingu.

Harambee Stars inacheza mechi zake Malawi kutokana na shughuli za ukarabati zinazoendelea katika viwanja vya Nyayo na Kasarani.

Kasarani, ambayo ina uwezo wa kuwasitiri mashabiki 60,000 inakarabatiwa kwa kipute cha Kombe la Afrika (AFCON) 2027.

Nayo Nyayo inatengenezwa ili kuandaa kipute cha CHAN cha wachezaji wanaocheza kwenye ligi za nyumbani ambacho kimepangwa kufanyika Septemba mwaka huu.

Kenya ilianza mechi ya Ijumaa kwa kishindo huku ikipoteza nafasi za wazi ambazo zingewazalishia mabao mapema.

Olunga alifanyiwa masihara nje ya kisanduku dakika ya 19 na akauchanja mpira huo wa ikabu ambao uligonga ukuta wa wanasoka na kurejea mchezoni.

Stars walikuwa ndio bora zaidi katika kipindi cha kwanza huku Burundi wakilazimika kudunga hema kwenye lango lao ili kuweka ulinzi mkali.

Mapema katika kipindi cha pili Burundi waliponyoka baada ya mnyakaji wao Jonas Nahimana na beki Derick Mukombozi kuokoa makombora mawili kutoka kwa Kenneth Muguna na Aboud Omar.

Kenya ilinusurika dakika ya 52 baada ya Bienvenu Kanakimana kumpita Rooney Onyango na kuachilia kombora kali ambalo iligonga chuma na kutoka nje huku Matasi akiwa upande mwingine wa goli.