Habari za Kitaifa

Mjane aomba mahakama iwaadhibu vikali waliomuua mbunge

May 29th, 2024 3 min read

NA RICHARD MUNGUTI

MJANE wa aliyekuwa Mbunge wa Juja George Thuo, Bi Judy Thuo, mnamo Jumanne aliomba Mahakama Kuu iwaadhibu vikali mmiliki wa kilabu cha Porkies na wafanyakazi wake watano.

Katika ripoti aliyowasilisha mbele ya Jaji Roselyn Korir anayesikiliza kesi hiyo, Judy amedokeza kwamba kifo cha mumewe kiliathiri familia yake mno na “waliohusika na kifo chake waadhibiwe vikali na kwa mujibu wa sheria.”

Judy aliomba mahakama itende haki ili maisha ya mume wake aliyekuwa akiwapenda yeye, watoto na watu wa familia yake yasiwe yalipotea bure.

Mjane huyo aliirai mahakama itende haki.

Mmiliki wa kilabu maarufu mjini Thika, Paul Wainaina Boiyo almaarufu Sheki na wafanyakazi wake watano waliopatikana na hatia ya kumuua Thuo mwaka 2013, watasubiri hadi Juni 21, 2024, kujua hatima yao.

Siku hiyo Jaji Korir atapitisha hukumu.

Jaji Korir aliamuru washtakiwa wazuiliwe katika idara ya magereza.

“Mume wangu hakuwa na uhasama na mtu yeyote. Alienda na hakurudi nyumbani. Alifia katika mikono ya watu aliokuwa nao kwenye kilabu cha Porkies. Naomba hii mahakama iwaadhibu wahusika. Maisha ya mtu hayawezi kupotea vivi hivi,” Judy alieleza mahakama katika ripoti aliyotoa kwa afisa wa urekebishaji tabia.

Jaji Korir aliyesikiliza kesi alikuwa ameitisha ripoti kutoka kwa wahasiriwa wa mauaji ya Thuo ambao ni mkewe, dada na ndugu zake na hata majirani.

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa na Mercy Kanyange, mahakama ilielezwa na wahasiriwa kwamba kifo cha Thuo kiliwaathiri kwa njia nyingi ikitiliwa maanani alikuwa mtu mkarimu.

Mahakama iliombwa na wahasiriwa hao ipitishe adhabu kali dhidi ya washtakiwa.

Lakini wakili mkongwe na mwenye tajriba ya juu Dkt John Khaminwa, ambaye amehudumu taaluma ya uwakili zaidi ya miaka 60, aliomba Jaji Korir akubaliane na Bi Kanyange na kuamuru washtakiwa watumikie kifungo cha nje.

Dkt Khaminwa alisema washtakiwa hawana hatia na “kusema ni vigumu watu sita kumtilia sumu katika kinywaji mtu mmoja.”

Jaji Korir aliwapata na hatia Boiyo, Christopher Lumbasio Andika, Andrew Karanja Wainaina, Samuel Kuria Ngugi, Esther Ndinda Mulinge na Ruth Vanessa Irungu, ya kumuua kwa kumnywesha sumu Thuo mnamo Novemba 19, 2013.

Punde tu baada ya kuwapata na hatia washtakiwa hao, Dkt Khaminwa alimweleza Jaji Korir, “Uamuzi huu wako umenishtua sana. Sikutarajia utawapata na hatia washtakiwa. Haiwezekani watu sita wamnyweshe sumu mtu mmoja.”

Baada ya sita hao kupatikana na hatia ya kumuua Thuo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga aliomba idara ya urekebishaji tabia iwahoji washtakiwa na familia ya marehemu kabla ya adhabu kupitishwa.

Akitathmini ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Jaji Korir alisema “washtakiwa wote walihusika kwa njia moja au nyingine katika kifo cha Thuo ambaye Dkt Khaminwa na mawakili wengine walisema alikuwa anahofia maisha yake.”

Jaji Korir alisema Thuo alikuwa ameorodheshwa kutoa ushahidi katika Mahakama ya Kesi za Uhalifu wa Kimataifa (ICC) yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi.

Rais William Ruto na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta walikuwa wameshtakiwa kwa kushiriki katika ghasia za baaada ya uchaguzi wa 2007 ambapo watu zaidi ya 1,000 waliuawa na wengine zaidi ya 600,000 kuhamishwa makwao.

Mawakili waliowatetea washtakiwa hao walisema huenda waliomtishia maisha Thuo ndio waliohusika.

Lakini Jaji Korir alitupilia mbali madai hayo na kusema washtakiwa ndio walihusika na kutia sumu katika pombe ambayo Thuo alimimina siku hiyo akitazama mchezo wa Formula One kwenye kilabu.

Mahakama ilisema Thuo aliaga dunia kutokana na kuvuja damu kwenye utumbo wake na machengelele.

“Boiyo na Andika walikuwa wamezugumza na Thuo kabla ya kutoka kwa nyumba yake. Wawili hao walikuwa na muda wa kutosha kumpangia hila au wema mwanasiasa huyo,” Jaji Korir alisema.

Aliongeza kusema wafanyakazi wawili wa Boiyo waliketi naye kwenye meza moja na hawakutoka muda huo wote hadi pale Thuo alipoanguka na kuzirai.

Kabla ya kuzirai, alikuwa amemweleza Boiyo kwamba anahisi joto kisha akaenda kutoa vesti ndani ya afisi yake na kuipeleka kwenye gari lake.

Alipofika kwenye kilabu, aliuziwa pombe na Ndinda na ukaguzi uliofanyiwa chupa za pombe na gilasi ulionyesha kulikuwa na sumu ambayo ilimuua Thuo.

Jaji huyo alisema Vanessa alimnunulia pombe Thuo kisha akamkumbatia na kumbusu hata mahakama ikashangaa “je busu hilo lilikuwa la kumsaliti jinsi Judas Iscariot alivyombusu Yesu kabla ya kukamatwa na hatimaye kusulubiwa?” Hiyo ni imani ya Kikristo.

Washtakiwa wanazuiliwa katika magereza ya Industrial Area na Lang’ata.