Habari Mseto

Mwanabloga Pauline Njoroge amtetea Kipchoge dhidi ya shutuma

February 12th, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MWANABLOGA Pauline Njoroge amemtetea Eliud Kipchoge akisema ni nguli huyo aliyetabiri mwanariadha Kelvin Kitum angevunja rekodi yake kwenye mbio za masafa marefu.

Alifanya hivyo baada ya mashabiki kumshukia nyota Kipchoge kwa kutuma rambirambi zake kwa marehemu Kiptum, wakimshambulia kwa madai kwamba hakuwahi (Kipchoge) kumpongeza chipukizi huyo alipovunja rekodi mwaka jana.

Lakini kulingana na mwanabloga huyo, madai ya wale wanaouza simulizi za Bw Kipchoge kukosa kumpongeza Bw Kiptum kwa kuvunja rekodi yake ni habari potovu.

“Kipchoge hakutoa pongezi kupitia mitandao ya kijamii. Alifanya hivyo kwenye mahojiano. Na katika mahojiano hapo awali, Eliud alisema kuwa Kiptum alikuwa na uwezekano mkubwa wa kuvunja rekodi yake. Alimtaja Bw Kiptum kuwa na kipawa na mtu mwenye roho safi. Baada ya Kiptum kuvunja rekodi ya Eliud, kwenye mkutano na waandishi wa habari alimmwagia sifa kijana huyo. Alikuwa amemuona Kiptum mapema zaidi, aliona uwezo wake na akampendekeza,” alisema Bi Njoroge.

Aprili 2023, baada ya Bw Kiptum kushinda mbio za nyika, katika sherehe moja ya uzinduzi wa magari aina ya Isuzu, Bw Kipchoge alimpongeza Kiptum akitaja kuwa rekodi zake zaweza kuvunjwa.

“Huwa nasema hivi, rekodi hizo zipo pale kuvunjwa. Nina imani kuwa Kiptum atafanya hivyo siku zijazo. Ni jamaa aliye na moyo mzuri,” alisema Kipchoge wakati huo.

Kiptum aliandikisha  historia baada ya kuvunja rekodi ya mbio za London Marathon Aprili 2023 kwa muda wa saa mbili, dakika moja na sekude thelathini na tano. Desemba 4, 2023 alishida mbio zingine kwa muda wa saa mbili, dakika moja na sekude hamsini na tatu.

Mwaka huu kuna mashidano ambayo ni zaidi ya mbio sita kuu za dunia zitakazofanyika, kulingana na sheria za wanariadha huwezi kukimbia zaidi ya mbio tatu kwa mwaka.