Habari Mseto

Polisi alivyoshambuliwa na dereva aliyemkamata kwa makosa ya trafiki Mirema

June 2nd, 2024 1 min read

NA STEVE OTIENO

AFISA wa polisi anauguza majeraha katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki baada ya kushambuliwa na dereva aliyemkamata kwa makosa ya trafiki na aliyekuwa akimsindikiza hadi kituo cha polisi cha Kasarani.

Rekodi za polisi zinaonyesha kwamba afisa huyo wa cheo cha koplo alikuwa kazini katika barabara ya Kamiti, kwenye makutano ya Mirema akielekeza magari wakati alipoona gari likigeuka ghafla katikati ya barabara na kuzuia waendeshaji magari wengine, jambo lililosababisha msongamano.

Afisa huyo akaenda kwa gari kubaini kilichokuwa kinaendelea. Lakini alipomuona afisa huyo akiwasili, dereva huyo alijaribu kutoroka na katika harakati, akagonga jiwe la ukingo wa barabara na akakwama.

Alipokuwa anajaribu kujinasua, polisi huyo aliingia ndani ya gari hilo kwenye kiti cha mbele cha abiria na kumuagiza dereva huyo kupeleka gari kwa kituo cha polisi.

“Walipofika mkabala na duka la Quick Mart, dereva alisimama ghafla na akachomoa sime (aina ya upanga mrefu) chini ya kiti. Polisi huyo alitoka nje ya gari kwa kuhofia usalama wake lakini dereva huyo alimfuata nje akimnyeshea mangumi na mateke,” ikasema sehemu ya ripoti.

Katika songombingo hiyo, afisa huyo alijikwaa na kuanguka kwenye mtaro, jambo lililompa dereva huyo fursa ya kumpiga zaidi na kusakanya mifuko na kuondoka na betri ya simu.

Afisa huyo aliokolewa na wananchi na akakimbizwa katika kituo cha matibabu cha Crestview Mother & Child Wellness Centre, Kasarani kupata huduma ya kwanza kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Mama Lucy Kibaki kwa matibabu zaidi.

Kufikia wakati wa kuandika taarifa hii, mshirika mmoja wa shambulio hilo aliyetambuliwa kama Peter Kiragu ametiwa mbaroni huku polisi wakizidisha juhudi za kumnasa dereva huyo ambaye angali mafichoni.