Makala

Polisi wanne wanyakwa kwa wizi wa Sh2.2m za mishahara ya wafanyakazi wa shule

June 9th, 2024 2 min read

NA RICHARD MUNGUTI

POLISI wanne waliokamatwa kwa wizi wa mishahara Sh2.2 milioni ya wafanyakazi katika shule ya msingi ya kibinafsi ya Rophine International School, watakaa rumande hadi Jumatatu mahakama itakapoamua ikiwa watazuiliwa kwa siku 14 kuhojiwa.

Hakimu mkazi mahakama ya Milimani Geoffrey Onsarigo, aliagiza Sajini Antony Ndegwa, Koplo Daniel Lekakeny Sunkuli, Konstebo Simon Macharia Maina, na Konstebo Antony Mwendwa wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Capitol Hill kilichoko Upper Hill, Nairobi.

Polisi hao watahojiwa pamoja na Young Wakhisi na Lukas Magoiga Chacha almaarufu Rama.

Polisi hao na raia hao wawili walitiwa nguvuni kufuatia kuibiwa kwa pesa za shule hiyo zilizoibwa kutoka kwa gari la mhasibu wa shule Bw Victor Peter Owino.

Bw Onsarigo alielezwa kwamba Bw Owino alienda katika Family Bank tawi la Utawala-Embakasi na kutoa Sh2,361,500 ili kulipa wafanyakazi mishahara.

“Baada ya kuchukua pesa hizo, Bw Owino aliziweka ndani ya gari lake lenye nambari za usajili KCE 535L. Alienda shuleni kisha akachukua Sh161,000 na kuacha zile nyingine kwa gari,” hakimu alielezwa na kiongozi wa mashtaka.

Shule hiyo iko katika eneo la Mihang’o, Embakasi katika Kaunti ya Nairobi.

Bw Owino, mahakama ilijuzwa, aliegesha gari hilo nje ya afisi ya shule.

Alishuka na kuingia ndani ya afisi akiwa na Sh161,000 na kuacha Sh2.2 milioni ndani ya gari.

Alifunga gari kabla ya kuingia afisini.

“Salaale! Pesa alizoacha ndani ya gari takriban Sh2.2 milioni hakuzipata aliporudi kuzichukua kulipa wafanyakazi. Zilikuwa zimeibiwa,” Bw Onsarigo alifahamishwa.

Bw Owino alikabiliwa na mshtuko mkuu na kupigwa na bumbuazi.

Bw Owino alipiga ripoti kwa polisi kisha uchunguzi ukaanza kufanywa.

Korti ilielezwa mnamo Juni 6, 2024, katika eneo la kuegesha magari katika kituo cha polisi cha Kasarani, maafisa wa kitengo cha uchunguzi wa jinai (DCI) walimtia nguvuni Sajini Ndegwa akiwa na Sh64,000, Koplo Sunkuli akapatikana na Sh5,000.

Konstebo Maina alipatikana na Sh49,000 na Wakhisi alipatikana na Sh350,000.

“Pesa hizi maafisa kutoka DCI walishuku ni hizo ziliibwa kutoka kwa gari la mhasibu wa shule hiyo iliyoko Mihang’o,” hakimu alifahamishwa.

Hakimu alielezwa washukiwa hao – Sajini Ndegwa, Koplo Sunkuli na Konstebo Maina – hawakuwa kazini siku hiyo ya Juni 6, 2024, walipokamatwa.

Baadaye walimtia nguvuni Chacha katika eneo la Njiru naye Wakhisi alikamatwa akiwa mtaani Huruma.

Washukiwa hao walitiwa nguvuni katika egesho la kituo cha polisi cha Kasarani na maafisa wa polisi kitengo cha DCI kutoka Nairobi Region na DCI Kayole.

Maafisa hao wanne wa polisi walizuiliwa katika kituo cha polisi cha Kayole ilhali Wakhisi na Chacha walizuiliwa katika kituo cha polisi cha Ruai.

Mahakama iliombwa iwazuilie washukiwa hao kwa siku 14 ndipo polisi wakamilishe uchunguzi sawia na kutazama video za kamera za siri katika shule hiyo kutambua jinsi gari la Bw Owino lilivyofunguliwa na waliolifungua.

Hakimu alielezwa makazi ya Wakhisi na Chacha hayajulikani na hivyo basi wanatakiwa kusalia rumande.

Inspekta Dominic Omondi anayechunguza kesi hiyo, alieleza mahakama anachunguza hatia za kula njama za kuiba, kuiba kutoka kwa gari lililofungwa na kupatikana na pesa zilizoibiwa.

Pia mahakama ilielezwa polisi wanachunguza taarifa za huduma ya M-Pesa za washtakiwa na kwamba maafisa wa upepelezi wanafanya juu chini kupata pesa hizo za mishahara zilizoibiwa.

“Wataalamu wa masuala ya kiteknolojia kutoka afisi za DCI watachunguza picha za CCTV kutoka shuleni mle na za washukiwa kulinganisha ili ibainike ni wao waliovunja gari la Bw Owino na kuiba mishahara,” Bw Onsarigo alifahamishwa.

Baada ya kukamilisha uchunguzi, faili itapelekwa kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kwa ushauri zaidi.

Bw Onsarigo aliamuru washukiwa wazuiliwe hadi Jumatatu atakapoamua ikiwa polisi watapewa muda wa siku 14 kukamilisha uchunguzi.

[email protected]