Habari za Kitaifa

Ruto aondoka nchini kwa ziara nchini Korea Kusini

June 2nd, 2024 1 min read

UPDATE: Rais awasili jijini Seoul, Korea Kusini Jumatatu kwa kongamano baina ya Bara Afrika na Korea Kusini. Kiongozi wa nchi alisafiri kwa ndege ya kibiashara ya Fly Emirates

NA MWANDISHI WETU

RAIS William Ruto anaondoka nchini Jumapili jioni kwenda kuhudhuria kongamano baina ya Korea na Afrika, linalofanyika jijini Seoul, Korea Kusini.

Mataifa ya Afrika yanatazamiwa kujadiliana na Korea Kusini kuhusu masuala ya umuhimu haswa kwenye nyanja za biashara, viwanda, muundomsingi na ubunifu wa nafasi za ajira.

Ziara hii inajiri wiki moja baada ya kiongozi wa taifa kufanya safari nyingine ya siku nne nchini Amerika alikokuwa ameitwa kwa Ziara ya Kiserikali na ambako alifaulu kupata mikataba ya mabilioni ya pesa, ikiwemo ujenzi wa barabara ya expressway ya Mombasa-Nairobi.

Hata hivyo alikumbana na mjadala mkubwa kuhusu gharama ya ndege ya kibinafsi aliyotumia kwa ziara hiyo iliyokisiwa kumeza zaidi ya Sh200 milioni.

Katika ziara hii ya Korea Kusini, Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed anasema Rais Ruto atakuwa na mashauriano ya moja kwa moja na Rais Yoon Suk Yeol kuangalia yalipofikia Makubaliano ya Ushirikiano ya thamani ya Sh132 bilioni waliyokubaliana Rais huyo alipozuru Kenya Novemba 2022.