Habari za Kitaifa

Ruto kutafuta mtu mwingine baada ya Kemosi kukataa kazi ya ubalozi wa Ghana

April 9th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

ALIYEKUWA mbunge wa Mugirango Magharibi, Bw Vincent Mogaka Kemosi, amekataa uteuzi wake kama balozi wa Kenya nchini Ghana.

Mbunge huyo alikuwa miongoni mwa watu walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu kama mabalozi wa Kenya katika mataifa tofauti ulimwenguni.

Watu hao wanahojiwa na Bunge la Kitaifa, ili baadaye kuidhinishwa kuhudumu katika nafasi hiyo.

Mnamo Jumanne, Aprili 9, 2024, Bw Kemosi aliiandikia Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni, akisema kwamba hatafika Bungeni ili kuhojiwa.

Alikuwa ametarajiwa kuhojiwa na kamati hiyo Jumanne.

Kwenye barua aliyoiandikia kamati hiyo, Bw Kemosi alitaja sababu za kibinafsi na kifamilia kama hali iliyochangia uamuzi huo.

Barua yake ilisomwa na mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw Nelson Koech, aliyekiri kushangazwa na uamuzi huo.

“Ningetaka kuwafahamisha kwamba sitafika mbele ya kamati hii kwa wakati na mahali palipotajwa kwa kikao cha mahojiano,” akasema kwenye barua hiyo.

Akaongeza: “Hili linatokana na masuala ya kibinafsi na ya kifamilia yanayonizuia kuchukua nafasi ya kuhudumu kama Balozi wa Kenya nchini Ghana, kulingana na uteuzi uliofanywa na Rais William Ruto mnamo Machi 9, 2024.

“Hivyo, ili kuokoa wakati wa kikao hiki muhimu cha Bunge, na kulingana na Sheria iliyotajwa, tafadhali fahamu kwamba barua hii ni tangazo la kutofika katika kikao hicho. Ninawashukuru kwa mwaliko,” akasema.

Hatua hiyo inamaanisha kwamba Rais Ruto atalazimika kumteua mtu mwingine kuchukua nafasi hiyo.

Kamati hiyo ililazimika kuahirisha kikao chake.