Akili Mali

Ufugaji ng’ombe wa kisasa wa maziwa unavyosaidia kuponya makovu ya ujangili

Na OSCAR KAKAI July 1st, 2024 2 min read

KWA Mwongo moja sasa, jamii za Pokot na Marakwet katika eneo la Kaskazini mwa Bonde ufa zimekuwa zikipigana na kuhusika kwenye wizi wa mifugo.

Eneo hilo la mpakani lilikuwa la vita na wizi wa mifugo ambapo maisha yalipotea kabla ya hali ya utulivu kurejea mwaka wa 2000.

Mwanzo mpya ulianza baada ya wakazi kuchoka na maovu hayo na jamii hizo mbili kuelewana kubadilisha maisha yao kijamii na kuichumi.

Hii ilianza mwaka wa 1998 baada ya mauaji ya watu wengi kutokana na mizozo kati ya jamii za Pokot na Marakwet. Huu ulikuwa mwito kwa wakazi kukomesha wizi wa mifugo kwa kushirikiana pamoja kupata fedha kutoka kwa mifugo.

Wafugaji wa eneo hilo waliacha kilimo cha mifugo wa kienyeji na kukumbatia mifugo wa kisasa na kuanza biashara ya kuuza maziwa suala ambalo limeimarisha amani, kuinua uchumi na maendeleo kupatikana.

Huku wafugaji wakiacha ng’ombe aina ya Zebu na kufuga zile za Friesian, kilimo cha kisasa kinawaundia pesa.

Wafugaji hao hupata angalau lita tano za maziwa kila siku na kuuza kwa Sh50 kwa kila lita na kuimarisha uchumi.

Kuwepo kwa kampuni ya kununua maziwa ya Brookside katika eneo hilo kumesaidia wakulima kuanzisha mitambo mingi ya kuhifadhi maziwa.

Kati ya maeneo ambayo ng’ombe hao hufugwa katika eneo la Pokot Kusini ni Kabichbich, Chepkono, Kipat, Ringring, Chesupet, Kaptabuk na katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet ni Kipkaner, Koibatek, Sambirir. Endo, Emmbobut, Kapchepsar, Kapsait, Tembu, Kaberewo na Chemulany.

Ng’ombe wa maziwa wanaofugwa na wakazi katika mpaka wa Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet. Picha|Oscar Kakai

Uzalishaji wa maziwa kwenye kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet umechangia maeneo hayo kukua kwa haraka.

Uekezaji katika kilimo cha maziwa na serikali hizo za kaunti na kampuni ya Brookside umeleta mazuri katika eneo hilo.

Wakulima kwa pamoja wanategengeza kati Sh600,000 na milioni moja kila siku kutokana na mazingira mema kwa mifugo hao.

Ujenzi wa barabara ya lami ya Kapenguria – Iten pia umefungua eneo hilo na kusaidia kilimo hicho huku wakulima wakisafirisha maziwa yao hadi sokoni.

Grace Cheposait mkulima ambaye hupeleka maziwa yake kwenye mtambo wa kuhifadhi maziwa wa Lelan Highland aliwacha kufuga ng’ombe wa zebu na kununua friesiani ambayo inamlipa vizuri.

“Mapato yangu ni mema kwa sasa baada ya kubadilisha mbegu ya mifugo. Hatuelewi kuhusu utovu wa usalama kwa sasa sababu tuko kwenye shughuli ya shamba. Ufugaji ng’ombe wa maziwa umeimarisha uchumi wa eneo hili,” anasema.

Bi Cheposait huuza maziwa yake kwa Sh48 kwa lita moja na hupata Sh4,000 kwa wiki mbili.
“Nina na uwezo kimaisha na kujipatia mapato kila siku baada ya kuuza maziwa kila siku,” anasema.

Anasema kuwa sasa yuko na uwezo wa kuwalipia wanawe watatu karo ambao wako katika shule za upili.
“Mimi hulipa karo kutoka kwa maziwa na nina uwezo wa kulisha familia yangu pana,” anasema.

Mkulima mwingine Kenneth Lomaipong anasema kuwa kilimo cha maziwa kimebalisha maisha ya wakazi ambapo wote kutoka jamii za Pokot na Marakwet wanapata fedha kutoka kwa kuuza maziwa.

“Wakazi hufanya biashara za kuuza maziwa na hakuna hata wakati wamezozana. Hatujawahi kusikia majangili wameiba ng’ombe wa kisasa,” anasema.

Bw Lomaipong anasema kuwa kumekuwa na zaidi ya wafugaji elfu kumi wa ng’ombe wa kisasa na wako na uwezo wa kupata maziwa mengi sababu wako na mitambo ya kuhifadhi maziwa zaidi ya  30 eneo hilo.

“Kilimo cha maziwa kimebadilisha eneo hili, kuimarisha maisha na kupunguza umaskini,” anasema.

Anasema kuwa wakulima wa eneo wanakusanya zaidi ya lita 22,000 za maziwa kila siku kutoka kwa lita 2,200 ambazo walikuwa wakisanya mwanzoni.

“Wakulima wameimarika kiuchumi tangu waanze ushirika,” anasema.

Bw Lomaipong anasema wakulima hao walianzisha ushirika na wakulima sasa wanaweza kupata fedha za karo ambazo hulipwa baadaye kuuza kwa reja reja.

[email protected]