Habari za Kitaifa

Viongozi wa polisi watakaoongoza operesheni nchini Haiti watajwa

Na KAMORE MAINA June 24th, 2024 1 min read

NAIBU Inspekta Jenerali wa Polisi Noor Gabow na makanda wa idara mbili za polisi wataongoza oparesheni ya kikosi cha polisi Wakenya kule Haiti.

Bw Gabow,  Mkuu wa Operesheni katika kitengo cha GSU Samuel Chebet na mwenzake wa Polisi wa Utawala (AP)  Geoffrey Otunge, watawaongoza polisi kutoka hapa nchini kurejesha utulivu nchini Haiti.

Wawili hao walifahamishwa kuhusiana na uamuzi huo na Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome. Mabw Chebet na Otunge ni makamanda wa ngazi ya juu katika idara ya polisi na kupewa jukumu hilo linatarajiwa kuwavunia hela na marupurupu tele.

Kando na hayo, polisi watakuwa wakipewa chakula na malazi ya bure wanapowajibika katika kusaidia kurejesha amani Haiti inayotawaliwa na magenge.

Makanda wa polisi pia wataruhusiwa kuabiri ndege bure bilashi kutoka Haiti hadi Kenya na watakuwa wakiruhusiwa kurudi kuzitembelea familia zao baada ya kila miezi sita.

Kila kamanda amepokezwa jukumu rasmi kulingana na barua ambazo walipewa na kutiwa saini na Bw Koome. Duru zinaarifu kuwa Mabw Chebet na Otunge wataongoza operesheni ya maafisa kutoka AP and GSU Haiti.

Bw Chebet anatarajiwa ataondoka nchini Jumatatu naye mwenzake amekuwa kati ya maafisa ambao wamekuwa Haiti kujifahamisha na jinsi hali ilivyo na atajiunga naye baadaye kuchapa kazi hiyo.

Makamanda hao wawili watakuwa wakipiga ripoti kwa Bw Gabow ambaye ni mshirikishi mkuu wa operesheni hiyo dhidi ya magenge Haiti.

Naibu huyo inspekta jenerali wa polisi atakuwa na afisi Haiti na pia Marekani.

Wiki jana, makamanda wa polisi kutoka Haiti walikuwa hapa nchini ambapo walikutana na Bw Koome na kuzungumzia mipango ya usafiri ya polisi hadi Haiti.

Makamanda hao waliondoka Nairobi Juni 19 na kusema kuwa walikuwa wameridhishwa na maandalizi ya Kenya kuongoza operesheni Haiti.