• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 5:55 AM
Haiti: Kenya ikae chonjo isiingie mtego wa Amerika

Haiti: Kenya ikae chonjo isiingie mtego wa Amerika

NA CHARLES WASONGA

KENYA inafaa kuwa mwangalifu zaidi inapojiandaa kutuma jumla ya maafisa 1,000 wa polisi kuwa sehemu wa vikosi vya Umoja wa Mataifa (UN) vya kulinda amani katika taifa la Haiti.

Hii ni kwa sababu nchi hiyo, iliyoko eneo la Caribbean, imesambaratishwa na wahalifu ambao wamelemea polisi wake wapatao 10,000.

Imeripotiwa kuwa jiji kuu la Haiti, Port-Au-Prince linatambuliwa duniani kama kitovu cha watekaji nyara, wauaji,  wezi wa magari, wabakaji, wezi wa mabavu miongoni mwa wahuni wengine wabaya zaidi.

Kenya inapanga kutuma polisi wake nchini Haiti wakati ambapo wahalifu hawa wanadhibiti karibu asilimia 80 ya jiji kuu.

Polisi wetu wanatarajiwa kushirikiana na walinda usalama kutoka mataifa mengine kupiga jeki juhudi za walinda usalama wa Haiti kupambana na wahalifu hao sugu.

Lakini huku Kenya ikisubiri idhini kutoka kwa Baraza Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kabla ya kutuma polisi wake Haiti Novemba mwaka huu, kuna maswali ambayo yanahitaji majibu.

Mbona Kenya itume polisi katika nchi hiyo ambayo uhalifu wake ulilemea mataifa yenye uwezo zaidi kama vile Amerika, Canada na Ufaransa?

Pili, ikiwa mara nyingi polisi wetu hulemewa na majangili katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya, watawezaji kupambana na wahalifu katika nchini ambako utawala wa kisheria umeporomoka?

Tatu, mbona Umoja wa Mataifa (UN) usipeleke wanajeshi wa kulinda usalama nchini Haiti jinsi inavyofanya katika mataifa ya Afrika yanayokumbwa na misukosuko?

Ni kutokana na ukosefu wa majibu kwa maswali kama haya na mengine, ambapo mashirika ya kijamii kama Amnesty International-tawi la Kenya, yamemtaka Rais William Ruto kubatilisha nia ya kutuma polisi wetu nchini Haiti.

Isitoshe, makundi ya wahalifu nchini Haiti, na wanaharakati wa haki za weusi nchini Amerika, wameripotiwa kupinga uteuzi wa Kenya kama kiongozi wa juhudi mpya za kuleta usalama huko.

Wanapinga kile wanachotaja kama hatua ya Amerika, na washirika wake, kutumia Kenya kuendeleza ukoloni mambo leo nchini Haiti.

Hii ina maana kuwa endapo Kenya itatuma polisi wake nchini Haiti Novemba mwaka huu, maafisa wetu watakabiliwa na wakati mgumu zaidi.

Huenda baadhi ya maafisa hao wakapoteza maisha yao katika nchini hiyo ya watu weusi.

Kwa hivyo, ushauri wangu kwa Rais Ruto ni kwamba atafute njia zingine za kujizolea sifa miongoni mwa viongozi wa mataifa yenye uwezo mkubwa duniani kama vile Amerika.

Kwa mfano, anafaa kupalilia urafiki huo kupitia njia za kibiashara badala ya njia hii ya kutumia polisi wetu kwenda kutuliza machafuko ambayo yamelemea Amerika, ambayo ndio jirani wa Haiti.

Kwa mfano, tayari Amerika imeshauri raia wake kuondoka Haiti ikihofia usalama wao.

Ni unafiki mkubwa kwa nchi hiyo kushauri raia wake kuondoka nchi, badala ya kutumia nguvu zake za kijeshi kurejesha amani na utawala wa sheria.

  • Tags

You can share this post!

Ujenzi wa barabara Lamu kukabiliana na Al-Shabaab  

Kitabu kuelimisha sheria za mazingira na kuyahifadhi  

T L