Michezo

Wakenya Kibor na Kibii watawala Stockholm Marathon

June 1st, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKENYA Marion Kibor na Fredrick Kibii wameibuka washindi wa mbio za Stockholm Marathon nchini Uswidi mnamo Jumamosi.

Kibor ametwaa umalkia wa mbio hizo za kilomita 42 kwa saa mbili na dakika 31 na sekunde 46, akifuatiwa kwa karibu na Sifan Melaku kutoka Ethiopia (2:32:54) naye Mkenya Ivyne Jeruto akafunga mduara wa tatu-bora (2:34:01).

Kibii aliibuka mfalme wa Stockholm Marathon kwa kuandikisha saa 2:14:17 katika umbali huo, akimaliza sekunde 13 mbele ya Robert Ng’eno (2:14:30), Benard Kipkorir (2:15:41), Kennedy Kipyeklo (2:15:53) na Abednego Cheruiyot (2:16:46) katika kitengo hicho ambacho Kenya ilifagia nafasi tano za kwanza.

Nafasi tatu za kwanza zilituzwa Sh125,977, Sh75,586 na Sh50,391, mtawalia.

Wakenya wengine ambao wamewahi kushinda mbio za Stockholm Marathon ni Esther Kiplagat (2001), Rita Jeptoo (2004) na Jane Onyangi (2016) nao wanaume ni Benson Masya (1997), Martin Ojuko (1998), Josphat Chemjor (2003), Joseph Riri (2004), Willy Korir (2008), Paul Kogo (2009), Joseph Lagat (2010), Benjamin Bitok (2014), Stanley Koech (2016), Lawi Kiptui (2018) na Felix Kirwa (2022).