Habari Mseto

Wakulima wa miwa waliosamehewa madeni wapinga ushuru mpya wa kusafirisha mazao

June 3rd, 2024 1 min read

VICTOR RABALLA NA LABAAN SHABAAN

WAKULIMA wa miwa wana mseto wa furaha na hofu baada ya kusamehewa madeni na kukabiliwa na mzigo wa ushuru katika pendekezo la kodi ya nyongeza ya thamani ya asilimia 16 (VAT) katika usafirishaji zao hilo.

Wakulima hawa wanahisi kupitishwa kwa kodi hii kutavuruga maendeleo yanayotarajiwa katika sekta ambayo imezongwa na changamoto za mapato kwa miaka mingi.

Shirikisho la Kitaifa la Wakulima wa Miwa Kenya (KNSF), limekashifu yaliyomo katika Mswada wa Fedha wa 2014 yanayowalimbikizia gharama ya ziada ya angalau Sh2 bilioni kwa mwaka.

Wasagaji miwa huzalisha jumla ya tani milioni 1.2 za sukari kila mwaka. Kwa hivyo, wakulima wa miwa wamebainisha kuwa kutoza VAT ya asilimia 16 ni sawa na kuwapokonya Sh164 milioni kila mwezi.

Mwenyekiti wa shirikisho hilo Ezra Okoth amesema pendekezo hilo ni ‘dhalimu na baguzi’  akidai wakuzaji wa miwa wamelengwa zaidi ya wakulima wengine.

“Tumelengwa na sheria ambayo haitumiwi katika uzalishaji wa mimea mingine,” aliteta.

Mswada huu umepelekwa kwa umma ili wananchi na washikadau watoe maoni yao kabla ya kutathminiwa na kupitishwa kuwa sheria.

“Ni muhimu kuzingatia kuwa gharama ya sasa ya uzalishaji ni kubwa na sekta hii ina matatizo chungu nzima,”  Bw Okoth alisema.

“Kuanzishwa kwa VAT katika usafirishaji wa miwa kutalemaza uzalishaji wa bidhaa hii muhimu.”

Vile vile, alionya kuwa kuruhusu sukari kutoka nje bila ushuru na kuongeza ushuru zaidi kwenye usafirishaji wa mazao ya kilimo si haki kwa maendeleo ya wakulima wa humu nchini.

“Kwa nini serikali ina nia ya kukuza kilimo cha miwa katika nchi nyingine na kuua kilimo cha wenyeji?” aliuliza.

KNSF inatoa wito ikitaka kutupiliwa mbali kwa pendekezo hilo ikidokeza kuwa utekelezaji wake utaathiri ufufuzi wa sekta hii yenye misukosuko.

Mwenyekiti wa Chama cha Miwa na Bidhaa Shirikishi (KASAP) Charles Atiang’ hata hivyo amefurahia ahadi ya Rais William Ruto ya kutoa Sh2 bilioni kustawisha sekta ya miwa.