Habari za Kitaifa

Wateule wa nyadhifa za ubalozi kumulikwa na wabunge kuanzia Aprili 4

March 24th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

WANDANI wa kisiasa wa Rais William Ruto, aliowateua kuwa mabalozi wa Kenya katika nchi mbalimbali za kigeni, sasa watafika mbele ya wabunge kuanzia Aprili 4 hadi Aprili 11, 2024, kutetea ufaafu wao kwa nyadhifa hizo.

Watu hao wakiwemo wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu wa 2022, watapigwa msasa na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mahusiano ya Kigeni.

Kamati hiyo inaongozwa na Mbunge wa Belgut Nelson Koech (UDA).

Katika tangazo lililochapishwa katika Saturday Nation toleo la Machi 23, 2024, Karani wa Bunge la Kitaifa Samuel Njoroge anaalika umma kuwasilisha taarifa na memoranda za ama kuunga au kupinga uteuzi wa watu hao 27 kushikilia nyadhifa hizo.

“Hii ni kulingana na hitaji la sehemu ya 6 (9) ya Sheria ya Uteuzi wa Umma (kwa idhini ya bunge) ya 2011 mtu yeyote, kabla ya kupigwa msasa kwa walioteuliwa, anaweza kuwasilisha taarifa au hatikiapo kwa Karani wa Bunge akipinga ufaafu wa mtu kushikilia afisi ya umma aliyoteuliwa kwayo,” akasema Bw Njoroge.

Taarifa hizo zinafaa kuwasilishwa kwa Afisi ya Karani wa Bunge kupitia anuani S.L.P 41842-00100, Nairobi, au ziwasilishwa kama barua kwa Afisi ya Karani wa Bunge, Majengo ya Bunge, Nairobi au kupitia baruapepe ya [email protected] ili zipokelewe kabla ya Aprili 2, 2024, kufikia saa kumi na moja jioni.

Miongoni mwa watakaopigwa msasa ni aliyekuwa Seneta wa Kisumu Fred Outa aliyeteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Misri, aliyekuwa naibu gavana wa Kisii Joash Maangi (Uganda), aliyekuwa Seneta wa Bomet Christopher Lang’at (Cote d’Ivoire) na aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Pokot Magharibi Lilian Tomitom (Zambia).

Wengine ni aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Kaskazini Vincent Kemosi (Ghana), aliyekuwa Mbunge Maalum Halima Mucheke (Uholanzi), David Kiplagat Kerich (Amerika), aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Mawasiliano (CA) Ezra Chiloba (Los Angeles, Amerika) na aliyekuwa Afisa Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) Peter Mathuki (Urusi) miongoni mwa wengine.

Bw Njoroge pia aliagiza kuwa wateule hao wanapasa kufika mbele ya kamati hiyo kupigwa sasa wakiwa na vitambulisho vyao vya kitaifa, stakabadhi za masomo na hati zingine hitajika.

“Aidha, wanapasa kuleta barua au stakabadhi za kuonyesha kuwa wanatimiza makatwa ya asasi zifuatazo: Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA), Bodi ya Kutoa Mkopo wa Kufadhili Masomo ya Juu (HELB), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP),” Bw Njoroge akaongeza.

Mnamo Alhamisi wiki jana, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula aliwafahamisha wabunge kwamba afisi yake ilipokea majina ya wateule hao 27 na kuyawasilisha kwa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Ulinzi, Ujasusi na Mashauri ya Kigeni itayarishe mpango wa kuwapiga msasa.