Habari

Zaidi ya walimu 100,000 wasio na ajira waomba nafasi 10,000 zilizotangazwa na TSC

October 18th, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SIKU 11 baada ya Tume ya Huduma za Walimu (TSC) kutangaza nafasi za walimu vibarua 10,030 katika shule za msingi na upili, tume hiyo imepokea maombi kutoka kwa zaidi ya walimu 100,000 kwa nafasi hizo chache.

Maombi 97,736 ni kutoka kwa wale walioomba nafasi kufundisha katika shule za upili huku 5,182 wakisaka nafasi katika shule za msingi.

Walimu 4,300 kati ya watakaoajiriwa watatumwa kufunza katika shule za msingi zinazokumbwa na uhaba wa walimu huku 6,000 waliosalia wakitumwa kufanya kazi katika shule za upili.

Wale wa shule za msingi watalipwa marupurupu ya Sh10,000 kwa mwezi huku wenzao watakaopelekwa katika shule za upili wakipokea Sh6,000 kila mwezi.

Watakaojiriwa katika shule ya msingi sharti wawe wamehitimu kwa cheti cha P1 huku wale wa shule za upili wanahitajika kuwa wamehitimu na angalau cheti cha diploma. Na wanaotuma maomba wawe kati ya umri wa miaka 24 na 35.

TSC ilisema kuwa malipo hayo yatatozwa ushuru wa mapato kwa usawa licha ya kwamba walimu hao watatumwa kuhudumu popote nchini ambako kutapatikana nafasi.

Kwenye taarifa wa vyombo vya habari TSC ilisema idadi ya waliotuma maombi kupitia tovuti yake ilikuwa juu zaidi kiasi cha kuvuruga mitandao yake.

Ukarabati

Hata hivyo, tume hiyo iliweza kuifanyia mitambo yake ukarabati ili iweze kupokea idadi kubwa ya wanaowasilisha maombi.

“Vilevile, tumeongeza makataa ya kupokea maombi kwa siku moja kutoka Jumatano, Oktoba 23 hadi Alhamisi, Oktoba 24,” TSC ikasema.

Ilitoa wito kwa wale ambao hawatuma maomba kufanya hivyo ndani ya siku saba zilizosalia, huku ikiwahikishia kuwa shughuli ya kuwaajiri walimu wanaohitajika itaendeshwa kwa njia huru na haki.

“Wanaotuma maombi wanaweza kutafuta usaidizi kwa kupiga siku kwa nambari 0202892050/0202892052,” TSC ikaongeza.

Mwaka 2018 bunge la kitaifa liliiruhusu TSC kuajiri jumla ya walimu 80,000 kama vibarua kama hatua ya kupunguza kero la uhaba wa walimu katika shule za msingi na za upili za umma.

Takwimu kutoka TSC zinaonyesha kuwa shule za msingi na za upili zinakabiliwa na uhaba wa takriban walimu 120,000.

Na kufikia sasa tume hiyo imesajili jumla ya walimu 180,000 waliohitimu lakini hawana ajira.