Habari za Kitaifa

Acheni kujipenda ilhali Wakenya wanaumia, viongozi wa dini na mashirika waambia Serikali


VIONGOZI wa kidini na wanaharakati wametaka uwajibikaji katika serikali huku raia wakiandamana kupinga Mswada wa Fedha 2024.

Kiongozi wa Kanisa la Kiangalikana Nchini (ACK) Askofu Jackson Ole Sapit Jumanne alisema utawala wa Kenya Kwanza umewalemea Wakenya kutokana na ushuru ambao wanalimbikiziwa kila kukicha.

“Idadi ya watu ambao hawana kazi na wanaopoteza ajira itapanda sana. Vijana sasa wamejitokeza kuandamana bila kuangalia maslahi au ukabila na huo ni mwelekeo hatari kwa usalama wa nchi,” akasema Askofu Ole Sapit.

Kiongozi huyo wa kidini alisema kuwa biashara tayari zimeathirika na kile ambacho serikali inastahili kufanya ni kudhibiti uchumi wa nchi.

Pia aliwataka viongozi wote wajizatiti kutimiza ahadi tele ambazo zilitolewa wakati wa kampeni za kura ya 2022 badala ya kuwa vibaraka wa wanasiasa wakuu kisha kuunga nyongeza ya ushuru.

Alionya kuwa ikiwa ushuru utaendelea, “watu watafunga maduka, idadi ya watozwa ushuru itapungua na hasara itapatikana.”

“Tutakuwa na kiwango cha juu sana cha ukosefu wa ajira. Itaongeza ukosefu wa usalama katika nchi hii na itafanya nchi hii kuwa ngumu kutawala wakati watu wana mapato madogo,” alionya Askofu Mkuu Ole Sapit.

Alikuwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 5 la Kitaifa la Huduma za Maendeleo ya Kianglikana (ADS) jijini Nairobi alipowataka Wabunge kuwa waangalifu na kuelewa ukweli kwamba Wakenya tayari wamekwama kiuchumi.

Sapit alishauri serikali kuleta utulivu wa  kiuchumi, kisiasa na kijamii nchini kuepuka mzozo.

Kulingana naye, chochote kinachogusa utoshelevu wa chakula kinagusa usalama wa kawaida. “Kwa sababu wakati mapato yanapungua, watu wanatafuta njia zingine za kuishi, ikiwa ni pamoja na uhalifu.

Aliongeza: “Kwa sababu ni lazima serikali iendeshwe, lazima tuwe na bajeti yenye uhalisia. Ushuru dhalimu haukubaliki. Ushuru wa aina hiyo utawadhuru Wakenya.”

Wakati huo huo, Vuguvugu la Green Belt Movement (GBM) lilitaka uwajibikaji, likisema “kuna uhakika mdogo kwamba fedha zitapatikana kupitia hatua mpya zilizopendekezwa katika Mswada wa Fedha zitatumika kwa uwajibikaji na kwa malengo yaliyokusudiwa.”

Mswada tata wa Fedha unaopendekezwa unalenga kutoa hatua za ushuru ambazo, kulingana na GBM, zitaathiri tabaka la watu wa kipato cha chini na cha kati.