Maoni

Atwoli aruhusu Fazul akague matumizi ya fedha za ‘masoja’

April 26th, 2024 2 min read

Na CHARLES WASONGA

LENGO la kwanza la Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU), kulingana na maelezo kwenye tovuti yake, ni kuinua hali ya kijamii, kiuchumi na kisiasa ya wafanyakazi wote nchini.

Aidha, muungano huo unasema shughuli zake zote huwa zinalenga kuangazia matakwa ya wafanyakazi katika ngazi ya kitaifa, kanda na kimataifa.

Isitoshe, COTU hulenga kuendeleza mipango ya kuwaelimisha wafanyakazi kuhusu kuhusu masuala yanayohusu haki na mahusiano yao na waajiri wao.

Kimsingi, ni wajibu wa COTU kuvisaidia jumla ya vyama 45, wanachama wake, ili viweze kutetea masilahi ya wanachama wao katika kuhakikisha wanapata malipo yanayostahiki kwa huduma wanazotoa.

Wafanyakazi, ambao ni wanachama wa vyama hivyo, hulipa ada kila mwezi kwa vyama hivyo; pesa zinazotumika kufadhili shughuli zao.

Sehemu ya fedha hizo pia huwasilishwa kwa Cotu kufadhili shughuli zake zinazolenga kutimiza maono na malengo yake.

Ni wajibu wa vyama hivyo kutumia pesa hizo kwa njia inayoendeleza ajenda ya kutetea masilahi ya wafanyakazi bali sio masilahi ya maafisa wa vyama hivyo.

Lakini ni siri iliyo wazi kuwa kumekuwepo na visa ambapo maafisa wa vyama hivyo wametuhumiwa kufuja au kutowajibikia matumizi ya pesa hizo ambazo ni zao la jasho la wafanyakazi.

Ni kwa sababu hii ambapo zoezi linaloendeshwa na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Ulinzi wa Kibinafsi (PSRA) ya kukagua matumizi ya makato kutoka kwa mishahara ya walinzi wa kibinafsi yanayowasilishwa kwa vyama vya kutetea masilahi yao ni lenye mashiko.

Sekta zingine zinafaa kuiga mfano huu.

Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli, ambaye hujinadi kama mtetezi nambari moja wa masilahi ya wafanyakazi hafai kupinga shughuli kama hii bali anafaa kuiunga mkono.

Afisa Mkuu Mtendaji wa PSRA Fazul Mohammed, hajakosea anaposema kuwa ni wajibu mamlaka inayoongoza ni kuhakikisha kuwa michango ya kila mwezi ya jumla ya walinzi 1.3 yanatumika vizuri na Cotu.

Chama cha Kitaifa cha Kutetea Masilahi ya Walinzi wa Kibinafsi (KNPSWU) pia kinapaswa kuwajibikia fedha ambazo hupokea kila mwezi kama michango ya wafanyakazi wa kampuni mbalimbali za kutoa huduma za ulinzi wa kibinafsi.