Habari za Kaunti

Familia yaomboleza jamaa yao aliyeuawa na ‘teargas’


VIJANA walipojitokeza kuandamana dhidi ya Mswada wa Fedha 2024/25 katikati mwa jiji la Mombasa Jumanne, familia ya Emmanuel Giggs Tata, 20, haikuwahi kufikiria angekuwa sehemu ya takwimu za watu waliopoteza maisha yao katika maandamano hayo.

Emmanuel alikuwa na wenzake katikati ya mji wa Mombasa, dakika chache kabla ya polisi kuwafyatulia vitoa machozi ili kutawanya waandamanaji.

Kulingana na Bw Mwasa Nzamba, ambaye ni binamuye marehemu, kifo chake kilitokea muda mchache baada ya Emmanuel kuamua kurejea nyumbani kwao.

“Polisi walitupa vitoa machozi kutoka pande zote, walikuwa wametuzingira. Ni hapo ndipo Giggs hakuweza kutembea tena kwani hewa ilikuwa imeingia kwenye mapafu yake, na kumsababishia ugumu wa kupumua,” akasema Bw Nzamba.

Kulingana na babake Emmanuel, Bw Paul Tata, mwanawe alikuwa amerejea nyumbani kutoka chuo cha kitaifa cha mafunzo ya kiufundi cha Meru. Alieleza kuwa alikuwa akijaribu kukusanya fedha za kuhakikisha anarejea chuoni Julai.

“Ningependa kumwomba Rais William Ruto kuzungumza na vijana. Nimemlea Giggs kwa kujikakamua pamoja na dadake. Nilikazana ili afike chuo kikuu, ila sasa maisha yake yamekatizwa akiwa mwaka wa pili. Alikuwa rafiki yangu na siyo tu mwanangu,” akasema Bw Tata, akipandwa na hisia za kumpoteza mwanawe, ambaye alimpa jina la aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Manchester United Ryan Giggs.

Familia hiyo sasa inaomba serikali na wasamaria wema kuisaidia kumpatia mwana wao mazishi ya kufaa.

Katika Hospitali Kuu ya Mafunzo na Rufaa ya Pwani (CGTRH), watu kadha walilazwa wakiwa na majeraha ya risasi.

Taarifa kutoka kwa maafisa ndani ya CGTRH zilifichua kuwa kufikia Jumanne jioni mtu mmoja alikuwa ameaga pindi tu baada ya kufika hospitalini humo, mwingine akilazwa katika kitengo cha kushughulikia wagonjwa mahututi. Walieleza kuwa wengine tisa walikuwa wakiuguza majeraha ya risasi.

“Walikuwa na majeraha ya risasi, wengine kwenye shingo, wengine kwenye mikono na sehemu zingine za mwili. Viwango vya hatari vilikuwa vinategemea sana ni wapi walikuwa wamepigwa risasi,” akasema afisa huyo aliyeomba kutotajwa kwa kukosa mamlaka ya kuzungumzia suala hilo kwa umma.

Alieleza kuwa, majeruhi kadha walikuwa wamevunjika mifupa kutokana na risasi, hasa wale waliopigwa risasi kwenye miguu na mikono.

Mwanamume aliyejeruhiwa ambaye aliomba kutotajwa kwa hofu ya kuhujimiwa, alieleza kuwa simu yake ya mkono ilimwokoa baada ya kufyatuliwa risasi mara kadha. Alikuwa amepigwa risasi kwa mkono na paja, ila simu yake ikapokea athari ya risasi moja.

“Hadi sasa simu yangu ina mabaki ya risasi,” akasema.

Mwathiriwa mwingine, Bw Jonah Shikoli, 21, aliponea chupuchupu baada ya kupigwa risasi mgongoni.

“Nasubiri kurejea kwenye chumba cha upasuaji kutolewa risasi iliyosalia ndani ya mwili. Inauma kuwa polisi walitumia risasi kwetu, ninachoomba ni amani,” akasema.

Alieleza kuwa mwenzake waliokuwa pamoja katika ambulensi wakilelekea hospitalini alifariki walipofika hospitalini.

Gavana Abdulswamad Nassir alithibitisha watu 11 walikuwa wamefikishwa hospitalini na majeraha ya risasi, akasema kaunti itagharamia matibabu yao.