Kimataifa

Iran kuingia debeni Juni 28 kufuatia kifo cha Raisi

May 22nd, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

TEHRAN, IRAN

JUNI 28, 2024, imeidhinishwa kama tarehe mpya ya uchaguzi wa urais nchini Iran baada ya kifo cha Rais Ebrahim Raisi katika ajali ya ndege mnamo Jumapili.

Tarehe hiyo ilipitishwa wakati wa mkutano wa wakuu wa mihimili mikuu ya serikali.

Kulingana na makubaliano ya awali ya baraza la ulinzi, uchaguzi wa 14 wa urais utafanyika Juni 28, 2024, taarifa ya vyombo vya habari ilisema.

Haya yanajiri huku nchi hiyo ikiendelea kumuomboleza Rais Raisi aliyekufa kwenye ajali iliyotokea mpakani mwa Iran na Azerbaijan.

Mnamo Jumanne, msafara mkubwa wa kumuomboleza ulifanyika katika mji wa Tabriz, karibu na mahala ambapo helikopta iliyombeba ilianguka na kumuua Jumapili alasiri.

Maelfu ya watu walionekana kujitokeza kushiriki katika shughuli hiyo katika mji huo mkuu katika mkoa wa Azerbaijan Mashariki.

Misafara mingine kama hiyo inatarajiwa kushuhudiwa kote nchini Iran ndani ya wiki kadhaa zijazo.

Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anatarajiwa kuongoza ibada ya pamoja ya wafu katika jiji kuu Tehran baada ya msafara mwingine kufanyika katika mji mtakatifu wa Qom.

Licha ya watu wengi kujitokeza kwa misafara hiyo, maombolezo kote nchini Iran yamekuwa ya utulivu.

Raisi alipewa jina la lakabu ‘Mchinjaji wa Tehran’ kwa kudaiwa kuhusika katika mauaji ya kinyama ya wapinzani wa serikali katika miaka ya themanini (1980s).

Aidha, aliamuru operesheni dhidi ya waandamanaji dhidi ya serikali mnamo 2022 na mwaka 2023.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Amerika Matt Miller alisema “kuna damu mikononi mwa Raisi” kutokana na kuhusika kwake katika mchakato wa kuwazima wapinzani wa serikali.

Alimtaja marehemu ambaye zamani alikuwa kiongozi wa kidini mwenye msimamo mkali kama, “mshirika mkuu katika vitendo vya kuwakandamiza raia wa Iran kwa karibu miongo minne.”

Inadaiwa kuwa wanajeshi wa Iran walihusika katika mauaji ya mamia ya watu na kuwasukuma gerezani maelfu ya wengine kuhusiana na machafuko ya mwaka 2023.

Fujo hizo zilichochewa na mauaji ya mwanamke raia wa Iran aliyezuiliwa katika korokoro ya polisi kwa kosa la kutovalia vizuri vazi maalum la kusitiri uso, hijabu.

Licha ya uhasama na Raisi, msemaji wa Usalama wa Kitaifa katika Ikulu ya White House John Kirby mnamo Jumanne alisema taifa la Amerika lilituma risala za rambirambi kufuatia kifo cha kiongozi huyo.