Siasa

Jeshi la Gachagua lilivyomuacha kwa mataa

June 4th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Agosti 21, 2023, akihutubia washirika wa kanisa la Presbyterian la Gathiru-ini katika Kaunti ya Kiambu, Naibu Rais Rigathi Gachagua alisimulia jinsi yeye, Moses Kuria, Ndindi Nyoro, Kimani Ichungw’ah, Alice Wahome na Jayne Kihara walishirikiana kuzindua ukaidi wa kisiasa Mlima Kenya kwa manufaa ya ushindi wa Rais William Ruto.

Alisema kwamba mikutano ya kuzindua mikakati ya kumkaidi aliyekuwa kinara wa siasa za Mlima Kenya, Rais wa Nne wa Kenya Uhuru Kenyatta, iliandaliwa hata katika nyumba ya Bi Kihara iliyoko katika viunga vya mji wa Naivasha miaka miwili kabla ya uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Wanasiasa hao sita walianza kufahamika kama ‘Big Six’ na ambao walikuwa wamemkubali Bw Gachagua kuwa kinara wao katika vita hivyo ambavyo viliishia kuwa na ufanisi mkuu wa kumwezesha Rais Ruto kutwaa asilimia 87 ya kura za Mlima Kenya huku Bw Kenyatta akimsukuma Bw Raila Odinga kuukwea mlima huo akiangukia pua kwa chini ya asilimia 13.

Kama zawadi, Bw Gachagua—licha ya kupata kura tatu dhidi ya 27 za Kithure Kindiki katika mchujo wa mgombezi mwenza–aliishia kuwa Naibu wa Rais baada ya Dkt Ruto kumteua kwa ulazima, Bw Ichung’wa akawa kinara wa wengi katika bunge la kitaifa, Bw Nyoro akawa mwenyekiti wa kamati ya Bajeti, Bi Wahome akawa Waziri wa maji kabla ya kuhamishwa hadi ile ya ardhi huku naye Kuria akiteuliwa Waziri wa biashara na viwanda kabla ya kuhamishiwa hadi ile ya utumishi wa umma.

Ni Bi Kihara peke yake ambaye alibakia kuwa mbunge, Bi Wahome akijiuzulu kama mbunge wa Kandara ili kuwajibikia uteuzi ndani ya baraza la mawaziri.

Ajabu ni kwamba, leo hii hao sita hawaonekani kuwa na mshikamano waliokuwa nao wakimpangia njama Bw Kenyatta, Bi Kihara akionekana tu kuwa aliye na imani ya dhati kwa Bw Gachagua kama Naibu wa Rais na kinara wa siasa za Mlima Kenya.

Kwa mfano, Bw Kuria anaashiria hali ya wazi ya kutomtambua Bw Gachagua.

“Bw Gachagua ni mdosi wangu ndio na sijui ni kwanini unaniuliza kuhusu yeye… Lakini kitu cha kujua ni kwamba yeye sio chaguo letu la kuwasilisha shida za Mlima Kenya… Asiseme eti ako na ukiritimba wa kuwa nyapara wetu. Atakuwa nyapara kama nani?” Bw Kuria akahoji katika mahojiano ya wiki jana na runinga ya Citizen.

Bw Kuria amekuwa akitoa misimamo mikali inayoashiria kumpinga Bw Gachagua katika masuala mengi ya kiserikali.

Tayari, ameshasuta vita dhidi ya ulevi kiholela ambavyo Naibu wa rais anashirikisha ndani ya Mlima Kenya, kwa kuvitaja kama “visivyo na umakinifu wa kimawazo”.

Kuna madai yaliyozuka kwamba Bw Kuria alikuwa afutwe kazi kutoka Baraza la Mawaziri kabla ya 2024 lakini Bw Gachagua akajitokeza akisema “haendi mahali na atabakia ndani ya afisi… kile nitafanya ni kuongea naye ndio nidhibiti maongezi yake yakome ile nembo ya uasi na ukakasi”.

Kwa upande wake, Bi Kihara anasema kwamba hali ilikuwa shwari hadi pale kulianza kujitokeza mkono fiche wa kumhujumu Bw Gachagua katika siasa za kitaifa na za Mlima Kenya.

“Siamini yale ninayoshuhudia katika siasa za sasa ambapo Bw Gachagua anahujumiwa kila kuchao. Kuna mengi ambayo Bw Gachagua alitekeleza ndio tujipate ndani ya ushindi wa serikali tuliyo nayo. Ni utundu usioeleweka ukiandamana na usaliti wa kiwango cha juu kuwaona wale ambao walipata vyeo kutokana na bidii pamoja na rasilimali za Gachagua wakianza kumhujumu,” Bi Kihara akaambia Taifa Leo.

Alisema kwamba “kwa sasa kile ningehimiza wale tuliochaguliwa nao ndani ya Mlima Kenya ni kwamba kuna manufaa ya kudumisha ule umoja wetu kwa kuwa ndio nguvu yetu katika kusaka maendeleo kwa watu wetu na kuheshimika katika siasa za 2027 na 2032”.

Bw Nyoro ambaye amekuwa jina la kurejelewa kila wakati katika masaibu yake Bw Gachagua, tayari amesema kwamba yeye ni mtiifu kwa Rais Ruto na Bw Gachagua, akiongeza kwamba nafasi yake katika serikali ya hao wawili ni ile ya mtu wa mkono.

Hata hivyo, mshirika wake mkuu ambaye ni Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu, ametangaza kwamba anatarajia Bw Nyoro atuzwe wadhifa wa Bw Gachagua mwaka wa 2027 na hatimaye mbunge huyo wa Kiharu aibuke mrithi wa ikulu 2032.

“Wale ambao wanazingatia mengi ya kumtajataja Bw Nyoro watukome na wamuheshimu sawa na vile wanasema tumheshimu Bw Gachagua,” Bw Nyutu akasema Ijumaa akiwa katika Kaunti ya Kangema.

Bw Nyoro aliambia Taifa Leo kwamba hajawahi kunukuliwa akisema kwamba anataka au analenga kutwaa wadhifa wa yeyote.

“Wanaosema hayo pia wako na haki zao za kiutoa maoni na ni kawaida ya wanasiasa kuwa na misimamo yao ya kibinafsi,” akasema Bw Nyoro.

Kwa upande wake, Bi Wahome alisema kwamba katiba ya nchi imemfunga mdomo na hawezi kupiga siasa akiwa Waziri wa serikali.

Hata hivyo, alisema kwamba “ningetaka kuwaeleza kwa unyenyekevu kwamba maendeleo na uthabiti hukwepa popote palipo na mazingara ya malumbano…na ningewasihi mdumishe umoja”.

Bi Wahome alisema “sitaki kukumbuka yale ambayo tulipitia tukisaka serikali hii na kama shukrani yetu kwa Mola na wapiga kura wetu ni tuwe na heshima miongoni mwetu, tuzingatie manufaa ya wananchi na hatimaye tugange yetu ya kesho letu ndani ya mazingara ya utulivu pasipo kuraruana hadharani”.

Bw Ichung’wah aliteta kuhusu upenyo wa siasa za malumbano, ukabila na kupayuka ndani ya Mlima Kenya.

Licha ya kukwepa kujiunga na mrengo wowote wa malumbano hayo, Bw Ichung’wa ambaye analaumiwa kwa kuwa mwanamgambo wa vurugu ndani ya utawala wa serikali ya kaunti ya Kiambu alisema kwamba “sote tunafaa kumsaidia Rais Ruto kuafikia malengo yake ya kiutawala nasi tukimsaidia kukemea wale ambao hawana heshima na wengine na ambao hupora mali ya umma”.

Alisema “mimi niko katika mstari wa mbele kuhimiza hata serikali ya kwetu Kaunti ya Kiambu iwajibikie maadili mema ya kiutawala kama yanavyowekwa kama kielelezo na Rais Ruto”.

Alisema hakuna kiongozi ambaye anafaa kumzima mwingine kujieleza hasa katika safu ya kukimbizana na kuimarika kwa manufaa ya leo, kesho na kwa vizazi.

[email protected]