Siasa

Kalonzo aimarisha mikakati ya kutoshea kwa viatu vya Raila

March 1st, 2024 3 min read

CHARLES WASONGA Na MOSES NYAMORI

JUHUDI za kufufua mrengo wa One Kenya Alliance (OKA) zimeanza kujitokeza kufuatia mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa chama cha Kanu Gideon Moi mnamo Jumatano, hatua inayoweza kuwa pigo kwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

OKA ni sehemu ya Azimio chini ya kinara wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga ambaye ametangaza azma ya kugombea uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Hii imeibuka huku azma ya Bw Odinga ikizua hofu ya kuacha pengo la uongozi ambalo viongozi wa upinzani wanang’ang’ania kujaza.

OKA ya awali, iliwaleta pamoja kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, Bw Moi, Moses Wetang’ula wa Ford Kenya na Musalia Mudavadi, ambaye wakati huo alikuwa kiongozi wa Amani National Congress (ANC) kupinga mpango wa Bw Odinga kuwania urais 2022.

Sababu za kufufua mrengo wa OKA zinaakisi zile za kuelekea uchaguzi wa 2022 ambapo ulibuniwa kumtenga Bw Odinga na kumshurutisha kumuunga mkono mgombeaji mwingine wa urais.

Bw Moi Jumatano alimkaribisha Bw Musyoka, mwenzake wa Democratic Action Party – Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa na kiongozi wa chama cha Usawa Kwa Wote Mwangi wa Iria nyumbani kwake Kabarak kaunti ya Nakuru.

Watatu hao walilala mjini Nakuru kabla ya kuwa na maandamano mjini humo mnamo Alhamisi.

Taifa Leo imebaini kuwa mkutano wa Kabarak ulitanguliwa na mwingine kati ya Bw Musyoka na Bw Moi katika ofisi za kiongozi huyo wa Wiper SKM Center, Nairobi ambapo inasemekana walijadili uchaguzi wa 2027.

Bw Moi hajakuwa akihudhuria hafla za kisiasa – kufuatia kushindwa kwa Azimio na Kenya Kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Musyoka na Wamalwa wametangaza mipango yao ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi ujao na tangu wakati huo, wameanzisha juhudi za pamoja za kujipigia debe, huku wadadisi wakifichua mipango ya wawili hao kugombea urais pamoja Bw Wamalwa akiwa mgombea mwenza wa Bw Musyoka.

Watatu hao Jumatano walihudhuria Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti ya Homa Bay, ambapo Bw Musyoka alisema wazi kwamba yuko tayari kutwaa uongozi wa Azimio iwapo Bw Odinga atafaulu katika azma yake AUC.

Bw Musyoka aliwahakikishia wafuasi wa Azimio kuwa hakutakuwa na ombwe la uongozi katika muungano huo endapo kiongozi wake, Bw Odinga atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa AUC.

Bw Musyoka anayemezea mate kiti cha urais mwaka 2027 alisema kuwa atajaza nafasi hiyo ya Bw Odinga kuhakikisha kuwa upinzani unaendelea kuwa thabiti.

“Kuna wale ambao sasa wameanza kujihisi kama mayatima eti kwa sababu watamkosa ndugu Raila (Odinga) katika siasa za hapa Nyanza na katika ngazi ya kitaifa. Ningependa kuwahakikishia watu kama kakangu (Wycliffe) Oparanya kwamba ukimkosa Baba, mjomba Stevo yu hapa,” Bw Musyoka akawaambia wajumbe waliohudhuria Kongamano la Uwekezaji kaunti ya Homa Bay lililoandaliwa katika Chuo cha Tom Mboya.

Haya yanajiri wakati ambapo ndoto ya Bw Odinga ya kutaka kuwa mwenyekiti wa AUC inaendelea kuibua hisia mseto hasa katika chama anachokiongoza cha ODM.

Hata hivyo, Bw Kalonzo ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani, alitoa hakikisho kwa wafuasi wa Bw Odinga kwamba ataendelea kuongoza upinzani katika mkondo mzuri akipewa nafasi hiyo.

“Nadhani nimewahakikishia kuwa hamna ombwe katika uongozi wa Azimio na hamstahili kuwa na woga wowote,” akaeleza kiongozi huyo wa Wiper.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua, mshirika wa karibu wa Bw Musyoka aliambia Taifa Leo kwamba, Makamu huyo wa Rais wa zamani alikuwa akitumia mbinu zote ili kupata uungwaji mkono wa vinara wenzake katika azma yake ya kugombea urais 2027.

Alisema Bw Musyoka amekuwa akipanga mikutano ya pamoja na baadhi ya viongozi , ikiwa ni pamoja na Jumapili hii atakapoungana na Bw Wamalwa, Bw Iria na aliyekuwa Waziri Peter Munya kwa mkutano huko Embu.

“Kanu, ambayo inaongozwa na Gideon, ni chama tanzu cha Azimio. Kwa hiyo ni mshirika. Kiongozi wa chama chetu na washirika wake walilala mjini Nakuru na leo tulifanya mikutano miwili huko,” akasema Bw Wambua.

Aliongeza, “Hatutasubiri kuidhinishwa na mtu yeyote. Idhini pekee tunayotarajia ni kutoka kwa Mungu na watu. Watu wamekuwa wakituambia wanataka kumuona Kalonzo akizunguka nchi nzima; ndivyo tumeanza kufanya.”

Vilevile, Mbunge wa Kitui ya Kati Makali Mulu alisema baadhi ya washirika wao wa muungano huo, hasa ODM, wamemtendea vibaya Bw Musyoka baada ya baadhi ya washirika wa Bw Odinga kutoa masharti kabla ya chama hicho kumuunga mkono Bw Musyoka.

“Kiongozi wa chama chetu amekuwa mwaminifu na mvumilivu kwa Azimio na yeyote anayetupa masharti hamtendei haki. Tuko katika wakati hatujali ni nani anataka kumuunga mkono au la kwa sababu Kalonzo lazima awe kwenye debe,” akasema Bw Mulu.

Kwa kuwa Bw Odinga anapanga kuondoka katika ulingo wa siasa kulingana na hitaji la cheo ya AUC, baadhi ya viongozi ndani ya Azimio wameanza kujipanga kurithi wadhifa wa kiongozi wa chama hicho cha muungano.

Miongoni mwao ni manaibu kiongozi wa ODM, magavana wa zamani Ali Hassan Joho (Mombasa) na Bw Oparanya (Kakamega).

Hata hivyo, Bw Musyoka amemtaka Bw Odinga kulenga kuipa kipaumbele kampeni ya wadhifa wa AU badala ya siasa za kupinga serikali.

“Sasa Raila (Odinga) anahitaji kura ya Ruto na hawezi kusema ‘Zakayo shuka chini’,” Bw Musyoka ambaye ni mbunge wa zamani wa Mwingi Kaskazini akaeleza.

Tayari Rais Ruto ameelezea nia ya kumwidhinisha Rais kwa wadhifa wa AUC kwa kuanzisha kampeni ya kupigia debe miongoni mwa marais wa Afrika.