Jamvi La Siasa

Karata hatari ya Mudavadi kuvunja ANC na kuingia ndani ya UDA

Na MOSES NYAMORI June 22nd, 2024 2 min read

UAMUZI wa Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi wa kuunganisha chama chake unaweza kumweka kwenye hali sawa na aliyojipata awali iliyomfanya kusukumwa nje ya vyama alivyosaidia kuunda na ambavyo hangeweza kuvidhibiti.

Bw Mudavadi amekubali kuvunja chama chake cha Amani National Congress (ANC) ili kuungana na chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Rais William Ruto, na hivyo kujiweka katika hatari sawa na iliyompata hadi akaondoka katika vyama vya United Democratic Forum (UDF) na Orange Democratic Movement (ODM).

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wametaja hatua hiyo kuwa kama kamari inayoweza kumgharimu Bw Mudavadi kisiasa hasa azma yake ya kumrithi Dkt Ruto mwaka wa 2032.

Kuingia kwake katika chama tawala cha UDA pia huenda kukazidisha mzozo kati ya Rais Ruto na naibu wake Bw Rigathi Gachagua.

Kulingana na matokeo ya uchaguzi wa 2022, eneo la Mlima Kenya, ngome ya Bw Gachagua, ilipatia UDA kura nyingi ikilinganishwa na eneo la Magharibi la Bw Mudavadi, ambalo bado ni ngome ya kisiasa ya kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa UDA pia inaweza kukumbwa na laana ya vyama vikuu tawala vya zamani baada ya utawala wa Rais Ruto.

Chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta (JP) kilichoundwa kufuatia muungano wa vyama kadhaa kiligawanyika na umaarufu wake ukafifia.

Ingawa maafisa wa chama hicho walieleza kuwa vyama hivyo vitavunjwa na kuunda chama kipya, Taifa Leo imethibitisha kuwa UDA itabaki huku ANC ikivunjwa jinsi chama cha National Development Party (NDP) kilichokuwa cha Raila Odinga kilivyovunjwa na kumezwa na Kanu mwaka wa 2002.

Mudavadi amewahi kulazimika kujiuzulu

Bw Mudavadi amewahi kulazimika kujiuzulu kutoka kwa vyama vya siasa ambavyo alijenga kikamilifu.

Aliondoka UDF chama ambacho alitumia kugombea urais katika uchaguzi wa urais wa 2013 ambapo aliibuka wa tatu.

Bw Mudavadi aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama hicho kabla ya uchaguzi wa 2013 lakini akalazimika kujiuzulu mnamo Juni 2015 baada ya kung’ang’ania madaraka kwa zaidi ya mwaka mmoja na mwenyekiti wa chama wakati huo Hassan Osman.

Kabla ya kujiuzulu, Bw Mudavadi alikuwa amejaribu kuwatimua Bw Osman, na Seneta Boni Khalwale (Kakamega) na Martha Wangari (seneta maalum wakati huo) kutoka chama hicho bila mafanikio.

“Ninakushukuru sana kwa kuniruhusu kuwa mwanachama wa chama chako. Nakitakia chama heri katika juhudi zake za siku zijazo,” Bw Mudavadi alisema katika barua yake ya kujiuzulu iliyoandikwa Juni 2, 2015.

Baadaye alijiunga na ANC aliyoshirikiana na viongozi wengine wa upinzani kuunda National Super Alliance (NASA) hadi 2017.

Mnamo Desemba 2010, Bw Mudavadi alilazimika kujiuzulu kutoka kwa chama cha ODM cha Bw Odinga, chama walichoanzisha kufuatia kura ya maamuzi ya 2005.

Bw Mudavadi alijiondoa ODM ‘kwa sababu ya kushindwa kubadilisha sheria iliyomfanya Odinga mgombea urais moja kwa moja katika uchaguzi mkuu.

Mchanganuzi wa siasa, Bw Javans Bigambo, anasema mkakati huu wa kisiasa wa Bw Mudavadi unaweza kutatiza azma yake.

“Sio kila mtu katika ANC atamfuata Mudavadi hadi UDA. Wengine wanaweza kuchagua kujiunga na vyama vingine vinavyovutia zaidi na maarufu katika eneo la Magharibi. Mudavadi anaonekana kuingia katika muungano bila kushirikisha ipasavyo wanachama wa chama,” asema Bw Bigambo.

Anasema hatua hii huenda ikazua vita baridi kati ya Bw Mudavadi na Bw Gachagua kwani kila mmoja atataka kujiweka kwenye nafasi ya kumrithi Rais Ruto.

Kiongozi wa chama cha ANC, Bw Issa Timamy, alisema Jumatano kwamba chama hicho kinafahamu wasiwasi wa wanachama kuhusu muungano huo.

Lakini mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Bw Martin Oloo, anahoji kuwa rais Ruto anajua kwamba huenda Mlima Kenya hautampigia kura katika uchaguzi wa 2027 na amegeukia Magharibi na Nyanza kutafuta uungwaji mkono.