Maoni

MAONI: Kuangamiza pombe haramu kutafaulu tu iwapo uchumi wa Kenya utaimarishwa

February 12th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

VIFO vinavyotokana na unywaji wa pombe haramu yenye sumu kama vilivyotokea katika Kaunti ya Kirinyaga vimekuwa vikiongezeka kila siku.

Viongozi wamekuwa wakiahidi na kuapa kuangamiza upikaji na uuzaji wa vileo haramu ambavyo vimekuwa vikiua vijana.

Wanavyotoa ahadi hizi ndivyo watu wanapoendelea kufa kumaanisha kuwa mikakati inayotumiwa katika vita hivi haizai matunda.

Jambo moja lililo wazi ni kuwa vita hivi haviangazii chanzo halisi cha janga hili.

Ni janga kwa kuwa vileo haramu vimeripotiwa kuangamiza watu kote nchini wengi wakiwa vijana wenye nguvu za kuchangia ujenzi wa taifa. Kwamba wanakunywa vileo haramu ni kuonyesha hawana uwezo wa kununua pombe salama na hapa ndipo vita hivi vinafaa kuanzia.

Hatua ya kwanza ya kukabiliana na hali hii inafaa kuwa kuimarisha uchumi ili vijana wapate ajira na kulipwa mshahara mzuri.

Pili, serikali inafaa kuandama wanaotengeneza na kuuza vileo haramu ikiwa ni pamoja na maafisa wa utawala na usalama wanaoruhusu shughuli hizi kuendelea katika maeneo wanayohudumu.

Kabla ya kufanya hivi, ni lazima viongozi wajitakase wenyewe kwa kutowalinda wanaotengeneza na kuuza vileo haramu au wanaoingiza nchini pombe isiyoruhusiwa.

Hii ni kwa sababu wafanyabiashara wanaouza vileo haramu ni washirika wa watu wenye ushawishi serikalini wanaowalinda kwa hivyo kufanya kazi ya maafisa wa utawala kuangamiza uovu huo kuwa ngumu.

Si ajabu baadhi ya watu wanaopaza sauti wakilaani biashara hii wakawa wananufaika nayo huku nchi ikiendelea kupoteza raia wake.

Hivyo basi, kufanikisha vita dhidi ya pombe haramu kunahitaji zaidi ya kukamata wauzaji pekee. Vita hivi vinahitaji nia njema, ushirikiano na azima.

Bila kuimarisha uchumi, itakuwa vigumu kuangamiza uovu huu.