Makala

Nduguye Kabando ajutia kuua mamake akisubiri Msamaha wa Rais

June 12th, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO  Julai 27, 2014, familia ya aliyekuwa mbunge wa Mukurwe-ini Bw Kabando wa Kabando ilitumbukia katika lindi la msiba mkuu baada ya ndugu yake mdogo kumuua kwa kumkata shingo mama yao mzazi, Rose Wachera aliyekuwa na umri wa miaka 70.

Majirani nao wakiwa wamepandwa na mori kutokana na mauaji hayo waliingia katika boma hilo la kina mheshimiwa katika kijiji cha kijiji cha Ngamwa, Kaunti ya Nyeri na wakamkabidhi mshukiwa kwa jina Caesar Thiari Mwangi kipigo kikali.

Lakini polisi walifika kabla naye hajatumwa kwa kaburi na wakamwokoa Thiari.

Baadaye Thiari alishtakiwa kwa kosa la mauaji na akabaada ya kesi kukatwa, mwaka wa 2018 Novemba, alipatikana kwa hatia lakini akawekwa kwa kifungo cha msamaha wa rais (PP).

Kifungo hicho cha msamaha wa rais ambacho kwa kizungu hufahamika kama Presidential Pardon (PP), hutumika kwa aina mbili ya washukiwa, wale ambao walifanya hatia kuu wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 na pia kwa wale ambao walitekeleza hatia wakiwa katika hali ya kutojielewa kimawazo.

Akitekeleza mauaji hayo dhidi ya mamake mzazi, Thiari katika kujitetea dhidi ya kesi inayomsakama amekuwa akishikilia kwamba hakuwa na akili timamu kwa kuwa alikuwa ameharibikiwa na bongo lake baada ya miaka kadha ya utumizi wa dawa za kulevya na pia pombe.

“Mimi nilikuwa na ule uzoeefu mbaya wa mihadarati. Nilikuwa mvutaji wa bangi na sigara, mbugiaji pombe na pia mtumizi wa dawa nyingine hatari kama heroni na kokeni. Kwa uhakika haikuwa mimi bali ni shetani aliyekuwa akidhibiti akili yangu,” akasema akijitetea.

Kuzuiliwa kwake kunaweza tu kukapata afueni ikiwa Rais William Ruto au mwingine yeyote katika uhai wake, atatia saini msamaha na aachiliwe huru.

“Lakini kuna matumaini kwa kuwa ile kesi yangu ya kumuuliza Rais anisamehe itaamuliwa Juni 27, 2024, na niko na matarajio makuu kwamba huenda mahakama ione malilio yangu na ipendekeze kwamba Rais Ruto aniachilie huru,” Thiari akaambia Taifa Leo katika gereza la King’ong’o lililoko Kaunti ya Nyeri ambako anaendelea kuzuiliwa.

Thiari alisema kwamba amekuwa akiridhiana na familia yake “na hata ndugu yangu Kabando amekuwa akinitembelea hapa korokoroni na katika maongezi yetu, tumeshasameheana na hatuna kinyongo kamwe”.

Alisema kwamba akiwa gerezani, amekuja kujutia sana tendo lake la kumkatizia uhai mamake mzazi.

“Lakini nilikuja kuelewa baadaye kwa kuwa mimi nikisemwa kutekeleza unyama huo, sikuwa najijua wala kufahamu mazingira yangu,” akasema.

Alisema kwamba malezi yake katika eneo la Pwani ambako pia ndiko alisomea yalimpa ufahamu wa mitandao ya mihadarati na hatimaye katika maisha yake ya baadaye, akajipata kwa uraibu ambao kwa sasa anasema amepambana nao katika miaka yake 10 ndani ya jela.

“Kwa sasa sina huo uzoeefu. Ninajielewa sana na hata wakubwa wa hili gereza wamenipongeza kwa dhati kwa ujasiri wangu wa kuchukua hatua ya kubadilika na kuwa na nidhamu ya hali ya juu,” akasema.

Ajabu na kinaya ni kwamba, Thiari alitekeleza kitendo hicho cha mauaji kwa shinikizo la mihadarati wakati pia alikuwa kwa kusomea na kuhitimu, mshauri nasaha mkuu wa kiwango cha meneja katika taasisi mojawapo ya kusaidia waathiriwa wa mihadarati kurekebika.

“Nilikuwa mshauri katika asasi kadha katika Kaunti za Nakuru, Nyandarua, Homa Bay na Kiambu huku jukumu langu likiwa ni kuwashawishi wengine wasiwahi kuthubutu kuanguka katika shimo la mihadarati. Lakini mimi nililianguka mwenyewe nikiwa nimeshika Biblia yangu ya ushauri kwa wengine,” akasema.

Alisema kwamba baada ya kupona uraibu huo akiwa ndani ya jela ndipo alikuja kuelewa kwamba alitekeleza kitendo cha unyama cha “kumkata mamangu shingo nikitumia upanga na huwa najutia sana”.

Alishauri watumizi wa mihadarati popote walipo wajue “uraibu huo hukukosesha mianya tele ya kujiendeleza” na hatimaye unamwingiza mwathiriwa kwa shimo kama hilo.

“Mtu akiwa kwa shimo nililo ndani yake, hali ya kujinusuru huwa ni karata ya pata potea,” akasema.

Thiari alisema kwamba ikiwa atatoka jela, atakuwa mtiifu kwa sheria.

“Aidha nitalenga kumalizia kuchapisha kitabu changu ambacho nakiandika kwa kichwa ‘Nilipoteza Yote lakini Nikajipata’.

[email protected]