Habari za Kitaifa

Mwendo wa kasi wa matatu wasababisha ajali na kuua 11

Na TOBIAS MESSO June 30th, 2024 1 min read

WATU 11 walifariki katika ajali mbaya ya barabarani baada ya matatu ya abiria 14 waliyokuwa wakisafiria kuanguka katika eneo la Ratili kwenye barabara ya Narok-Bomet Jumamosi jioni.

Wengine wawili wanapokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Longisa ambapo walikimbizwa kuhudumiwa.

Kulingana na Kamanda wa Polisi Kaunti ya Narok Riko Ngare, ajali hiyo ilisababishwa na kupasuka kwa tairi huku manusura wakisema dereva alikuwa akiendesha kwa mwendo wa kasi.

“Dereva wa matatu ya kampuni ya Narok Safaris Shuttles Limited, iliyokuwa ikisafirisha abiria kutoka Narok hadi Bomet, alishindwa kulidhibiti gari hilo baada ya tairi kupasuka, likatoka nje ya barabara na kubingiria mara kadhaa na kusababisha vifo vya watu tisa papo hapo, ” Bw Ngare aliambia Taifa.

“Dereva, watu wazima wanane; wanaume sita na wanawake wawili walikufa papo hapo na mtoto aliyekuwa miongoni mwa waliokimbizwa hospitalini pia alifariki,” Bw Ngare alieleza.

Muuguzi katika Hospitali ya Longisa aliambia Taifa Leo kwamba mmoja wa watu wazima wawili wanaume ambaye alipata majeraha mabaya mengi, alifariki alipokuwa akipokea matibabu.

Miili ya marehemu ilipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali hiyo.

Gari hilo ambalo lilikuwa limeharibika vibaya, lilivutwa hadi Kituo cha Polisi cha Ololulunga