Habari za Kitaifa

Ndoto kubwa ya Ruto kwa bara la Afrika

May 31st, 2024 2 min read

NA AGGREY MUTAMBO

RAIS William Ruto ameendelea kushinikiza mabadiliko makubwa barani Afrika huku akihimiza Umoja wa Afrika (AU) ufanyiwe mabadiliko ili kuimarisha utendakazi wake.

Akiongeza juzi katika hafla ya ufunguzi wa Mkutano wa Kila Mwaka wa Benki ya Maendelea Afrika (ADB) katika ukumbi KICC, Nairobi, Dkt Ruto alisisitiza kuwa sharti AU ifanyiwe mabadiliko.

“Tutapendekeza kwamba maafisa wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) wapewe mamlaka ya kutosha ili kuendesha diplomasia ya kuichumi barani ndiposa tutumie vizuri rasilimali tulizo nazo kujenga Afrika bora kwa manufaa yetu sote,” akaeleza.

Alisema kuwa sharti AU iwe na nguvu ili iweze kupanua biashara kwa kulenga soko la Waafrika kwanza, ihakikisha miradi ya Afrika inafadhiliwa na asasi zake za kifedha, istawishe miundo msingi Afrika ili kuchochea maendeleo na ihakikisha kuwa Waafrika wanapata kupitia mahakama yao mahsusi.

“Umoja wa Afrika lazima usimamie usalama wetu, ulinzi na uthabiti wa bara hili. Sharti AU itusaidie kusuluhisha mapigano katika bara letu. Hatuwezi kupiga hatua kimaendeleo ikiwa kuna vita katika mataifa ya Sudan, Somali na misukosuko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tunahitaji mageuzi katika AU ili kuiwezesha kutuhudumia vizuri,” Dkt Ruto akasema.

Hii sio mara ya kwanza wa Rais Ruto kuukosoa umoja huo wa Afrika.

Lakini wakati huu anaukosoa AU kama mwenyekiti wa Kitengo cha Mabadiliko ya Kitaasisi katika AU, wadhifa ambao amerithi kutoka kwa Rais wa Rwanda Paul Kagame.

Kagame alipoondoka katika wadhifa huo Februari mwaka huu, alikiri kuwa baadhi ya asasi za AU zinaonyesha tabia ya kudharau sheria na taratibu kiasi cha kukaidi mwongozo kutoka kwa viongozi wa mataifa wanachama.

“Maamuzi yaliyofikiwa katika kiwango cha Viongozi wa Nchini yanaendelea kuangaliwa upya na kufanyiwa mabadiliko au hata kukataliwa na baadhi ya wanachama wa Kamati ya Kudumu ya Wawakilishi katika AU,” Rais Kagame akasema katika ripoti ya mwisho aliyotoa Februari.

“Aidha, tunaona asasi sambamba zikiundwa, ambazo lengo lao kuu ni kuhujumu au kuchelewesha mageuzi ambayo Marais na Viongozi wa Nchi walipendekeza yawekwe.”

Lakini kulingana na Ruto, asasi zote za AU zinahitaji kufanyiwa mageuzi ya kuziboresha.

Kwa mfano, alipendekeza kuwa Idadi ya Wabunge wa Afrika ipunguzwe kutoka 275 hadi 100.

Aidha, alipendekeza kuwa mamlaka ya Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) yafanyiwe mageuzi ili iweze kutekeleza majukumu mengi zaidi.

Mwaka 2023, Rais Ruto alipendekeza kuwa nyadhifa za Mwenyekiti wa AU na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Hii ina maana kuwa kiti cha AUC ambacho washikilizi wake hubadilishwa kila baada ya miaka minne huenda kikafutiliwa mbali.

Kwa hivyo, AU itaiga Umoja wa Ulaya (EU) yenye tume ya mamlaka zaidi ambayo inaweza kujadili mikataba ya kibiashara itakayotumika na nchi wanachama kando na kuwa na mamlaka ya kushughulia masuala kama vile amani, usalama na sera za kigeni za mataifa wanachama.